Wosia
Wa Babu
Furaha iliyo’je kuwa kwenye kigonda changu wakati kama huu wa magharibi?. Ha! Ha! Ha!...
Siniulize mbona nimekenua ‘ivo, ipo siku katika umri huu wangu, utaijua sababu.
Eti watamani kujua sasa ‘ivi?, aha! basi ni hivi, wapo wenye imani kuwa kuishi
ni lazima almuradi keshazaliwa. Kubugia chumvi si sheria. Ni kwa kudura zake tu
Rabana. Kupata dakika ‘izi za kusema nanyi wajukuu wangu, si kwa umri wangu, si
kwa uwezo wangu, si kwa utajiri wala uchochole wangu. Ni majaliwa yake Jalali!.
Wazazi wangapi haswa akina baba wanaotenga angaa
sekunde kadha kuwa na wana’o?, wangapi wanawanasihi watoto wao?... Jibu
utakavyo ila fahamu ukweli upo wazi.
Oooooh!, nimekumbuka, hata sijawasabahi. Hujambo
Hari?… vyema, sauti yako ina uvalana ndani yake. Sina shaka huwavutia sana
wasichana kama huyu dada’ko Sabina. Sabina hujambo?... Shukran’ kwa kuzipokea
salamu zangu. Kusudi la kuwaita hapa kwangu ni ili tuambizane yanayotuhusu.
Pakiwa na lakuuliza, ni hapo baadaye.
Mwanzo naomba mtafakari juu ya maisha kwa jumla. Maisha
ni ngazi. Maisha ni milima na mabonde. Maisha ni ndia telezi tena yenye ukavu
wake. Kila mtu ana maisha yake lakini sote tuna hatima moja tena sawia. Wapo
wenye mali na wajitambuao kama masikini, lakini juu ya yote, hamna tajiri wala
masikini. Sote twala mwande kuchapo hadi jua
lituapo.
Mmmmh!, huenda hamnielewi vilivyo. Nitawapa kisa
kimoja ili kuijenga taswira ya kitwndawili changu. Tangu nilipozaliwa na
marehemu mama’ngu, nimeyaona na kujifunza mengi. Tulikokuwa tukiishi zama hizo,
yaani Lodini, kuliwa kwa wakwasi tena wenye usemi. Familia yangu tu ndiyo
il’otafsiriwa kuwa masikini kabisa. Ilipigiwa
mfano kote.
“Mama”, ungekisikia kijitoto kikimwambia mama’ke,
“hiki chakula kimesalia nikipe mbwa au?”
“Mbwa?”
angebwata, “leo wajifanyahujui eh!, tangu lini mbwa wakala matapishi kama
hayo?, nenda kavitupe jaani. Wapo mbwa wenye njaa kuwazidi hawa wetu”… Eti
waulizaje Sabina?... Mbwa gani wengine isipokuwa aila yangu?. Usitwae
mwana’ngu.
Tulijaribu kutoshirikiana nao kwa
vyovyote vile lakini yote yalikwenda mvange. Si mwafahamu kuwa hamna mwenye
njaa anayejitosheleza?. Licha ya kuwa kitinda mimba katika familia ya watu kumi
na wawili, nilijitwika ya kuwalisha wakubwa wangu kwa kujishughulisha na
uzegazega. Ulikuwa uamuzi ul’onitoa shuleni licha ya kuwa nilienzi sana elimu.
Nguvu za kukazana na ugumu wa hali tulimokuwemo,
ziliwatoka wazazi wangu. Ndugu zangu wengine wakajihusisha na ulevi kwa
kisingizia umasikini... [itaendelea]
Haki zote zimenakiliwa na mwandishi
Haki zote zimenakiliwa na mwandishi
@dennis
2012
0 comments:
Post a Comment