Fasihi kama dhana, imeelezwa na wengi kwa kuegemea nadharia na mitizamo
mbali mbali. Hata hivyo ni muhimu tufahamu ya kwamba maana inayopewa dhana au
kitu fulani, huwa inachukuana na matumizi ya dhana yenyewe, watu wanaohusika,
mahali dhana hiyo inamotokea, na hata kipindi au wakati husika. Hii ndiyo sababu
twapata maana mbalimbali zikitolewa kuhusu fasihi. Kwa mfano, waandishi wengi wa
Kimagharibi wamesisitiza kwamba fasihi yahusu tu kazi zilizoandikwa.