MWANDISHI ADAM SHAFI |
Nimepokea simu. Simu ya
maana. Adam Shafi yuko Majuu. Kaja kikazi Uholanzi. Yeye mtaalamu wa lugha ya
Kiswahili. Baada ya kumaliza kapitia Uingereza katika mji mmoja wenye wakazi
wengi wa Kitanzania, yaani Milton Keynes. Ni wastani wa saa moja kwa treni toka
London. Mrefu, mchangamfu, mzungumzaji
aliyesheheni “mastore” kibao. Nishakutana na waandishi wa kila sampuli.
Wanaojificha: wakimya, wasioongea sana, wapole wanaokaa chumbani kati kati ya
watu ukadhani hawapo. Wanaopiga kelele, wakijafaragua; ama wenye aibu…
Shafi ni mtu wa kawaida
kabisa, naweza kuiita hulka, tabia na namna yake “Mfurahia Maisha” :
kachangamkia uhai, haswa. Kaishi,
anaishi…hamalizi. Kila mara atasema ana mikakati ya kufanya jambo fulani,
kuandika kitabu kingine kipya, kuendeleza fasihi na Kiswahili….
Katika saa nne zote
nlizokuwa naye ananikumbusha moja. Ikiwa umewahi kuvisoma vitabu vyake
utagundua huchanganya kila kitu: furaha, simanzi, vita, amani, mapenzi, karaha,
starehe, maonyo, mandhari, elimu na mengine tele. Ukiongea naye yuko hivyo
hivyo. Mastore kibao. Anaelezea namna wachapishaji waliotafsiri moja ya vitabu
vyake walivyotaka kumrusha fedha. Akawafungia safari hadi Paris kudai haki
hiyo. Au alivyofiwa na mpenzi wake wa ujanani zamaaaani…pamoja na mtoto.
Alivyotiwa jela ugenini ujanani (anamalizia kitabu kipya kuhusu kisa hiki, soma
mbeleni); alivyofungwa Unguja baada ya mauaji ya Rais Karume. Hadi leo mguu
wake wa kushoto ananionyesha bado una dosari (“pana ganzi pajani shauri ya
kulala sakafuni”); alifungwa miaka miwili. Visa, kibao. Vyote vimepenyezwa
angalau kiduchu ndani ya vitabu vyake. Vingine vishatafsiriwa lugha za kigeni.
Kimoja kilishinda tuzo. Niko naye. Tunakula ubwabwa uliopikwa vizuri na binti yake kwa nyama za
kukaanga…huku tukila huku tukiongea. Mazungumzo hayaishi. Ingawa masaa manne
mengi kukaa na mtu (kwa huku Ulaya ambapo muda ni dhahabu) nahisi itabidi
nipewe miezi ili kujua mengi zaidi ambayo nataka kuyafahamu. Anachonifurahisha
ni hii picha akiwa na mjukuu wake wa miaka minne. Huyu ni mtu aliyeshaishi.
Akaona mengi. Akazaa. Akalea. Aka…mcheki.
Waandishi ni watazamaji
na wasikilizaji wakubwa wa jamii. Waandishi ndiyo hutukumbusha yaliyotokea.
Kusingekuwepo waandishi tusingefahamu yaliyopita. Kila mmoja wetu kila siku
anahangaika na maisha. Tunaamka, tunakula, tunakwenda kazini au masomoni.
Tunarudi , tunalala, kesho yake hayo hayo: kila kukicha na kuchwa tunaona
mengi, tunayapita, tunayasahau. Ila waandishi? Wasanii? Kazi yao kuweka
kumbukumbu ya haya mambo. Kuyahadithia. Wapo waandishi wa aina nyingi. Wana habari.
Waandishi wa elimu na historia. Washairi. Watunzi wa muziki na nyimbo. Sinema.
Tamthiliya.Wapo waandishi wa fasihi kama Adam Shafi. Shafi alianza na kitabu
cha “Kuli”, kinachoelezea mgomo maarufu wa wafanyakazi maskini , Unguja mwaka
1948. Anasema alikuwa na miaka minane tu. Na ingawa anakumbuka juu juu tukio hilo utotoni, alikuja kuhaditihiwa na
mtu akaweka kumbukumbu na baadaye maandishini. (Unaona waandishi walivyo watu
muhimu, kutukumbusha?)
KULI
“Kuli” kilichapishwa na
Tanzania Publishing House (TPH) miaka ya Sabini. Lakini awali alichapisha “Kasr ya Mwinyi Fuad” ambacho
kimeshatafsiriwa lugha tatu za kizungu:
Kijerumani, Kifaransa na Kirusi.
Miaka ya karibuni,
Shafi kaibuka na “Vuta Nkuvute” kilichopata Tuzo kwenye tamasha la vitabu, Dar
es Salaam, mwaka 1998. Ni kisa cha mapenzi, tena mapenzi makali na mazito kati
ya msichana wa Kihindi na Mwafrika. Humo mna siasa na harakati za uhuru na
mengi mengine. Mseto mkubwa wa mapenzi na siasa, ambao si waandishi wengi wa
KIswahili wamemudu kuuchanganya.
“Vuta Nkuvute”
kilichapwa na Mkuki na Nyota. Soma habari zao hapa
Mwaka 2003 mwanafasihi
huyu alitoka na “Haini” ambacho kama anavyosema mwenyewe kiliogopwa na
wachapishaji wengi nchini. “Haini” si mchezo. Kitabu cha moto, cha kuchachafya.
Soma ukurasa wa kutisha wa mfungwa mmoja
akipambana na chatu, ukurasa wa 172:
“Anaiangalia dunia kwa
hofu na kukata tamaa, anachungulia kaburi. ..Alipomtazama yule chatu alimwona
anaanza kujinyumbua, ananyeka, kichwa amekiinua,kama anayezindukana kutoka
usingizini. Chakula chake amekwisha andaliwa, hana wasiwasi. Tayari kimo mle
chumbani.”
Kama desturi
visa vyote vya Shafi hujaa mateso, shida, majonzi, taabu za
Mwafrika; lakini haviishii na hisia hizi
za kukata tamaa na kutokwa machozi. Wahusika wake huteseka lakini mara
wakaibuka, wakaamka na kupambana na matatizo yao. Matumaini ndiyo rangi ya
suluhisho lake.
“…Moyo wa ujabali
ukamjaa tele akahisi na nguvu kama za simba yuko tayari kuvaana na chatu yule
kwa mikono yake miwili. Chatu naye amenyanyua kichwa anajiramba midomo. Huutoa
ulimi wake halafu akaurudisha ndani na
pale anapoutoa utadhani anatoa miali ya
moto kutoka mdomoni. Wanatazamana. “Nani atakayeanza kushambulia?” Haramia
anajuliza.”
Msomaji sin’takueleza
yaliishia wapi. Maana ukijua hutatamkiwa kitabuni. Nnachokumbuka sikulala baada
ya kusoma sura hii. Inatisha. “Haini” ni kitabu kinachosisimua sana.
Kilinikumbusha visa vya mwandishi wa Kimarekani Stephen King, ambaye karibu
vitabu vyake vyote vishafanywa sinema. Sinema yake maarufu ni ile ya kutisha
sana iitwayo The Shining. Sidhani ntakosea nikisema maandishi ya Shafi
hayapishani na waandishi wa aina hii hata kidogo. Vikitafsiriwa vitapendwa
ulimwenguni kote. “Haini” yahusu namna Shafi alivyofungwa jela miaka miwili akiwa
bado mwandishi wa habari (taaluma yake kikazi)…akifanya kazi gazeti la “Uhuru”
ambalo enzi za miaka ya Sabini (alipowekwa kizuizini) visiwani liliitwa “The
Nationalist.” Ubaya,walakini, mmoja. Kitabu hiki kimechapishwa Kenya na
Longhorn (http://www.longhornpublishers.com). Bongo hakipatikani kirahisi bali
duka moja tu mitaa ya Kinondoni.
Vitabu vyake vyote
Shafi vinaonyesha maisha ya sasa na yale yaliyopita. Anapenda kuhusisha
historia ya jamii. Kwa hivyo mbali na kustareheshwa unafahamishwa mambo yaliyopita
ya zamani. Hali hiyo imo pia katika muswada wake mpya “Mbali na Nyumbani” ambao
unaelekeza maisha ya ujanani wa mwandishi.
Kitabu Chake Adam Shafi |
Namsikiliza mwanafasihi
huyu aliyezaliwa Unguja mwaka 1940 akinisomea: “Mbali Na Nyumbani.” Anasema
huchukua wastani wa miaka mitano kumaliza kitabu kimoja. “Huwa sina haraka hata
kidogo…” Huandika kwanza kwa mkono halafu ndiyo akachapa katika tarakilishi
(kompyuta)….”Mbali na Nyumbani”
anafafanua, kinasimulia ujana wake kati ya mwaka 1960 na 1967 …akijaribu
kuvuka Afrika kwenda Ulaya. Hapa alipo ukurasa wa 427 (cheki picha
juu)anasimulia akiwa mpakani Sudan kuingia Misri. Anaposoma ananikumbusha mwaka
1978 nilipojaribu na mimi kustoawei kwa meli. Vijana enzi hizo tulitaka sana
kupanda meli. Ubaharia ulikuwa kazi ya kutamanika, kutafutwa na kuotea. Miaka
hiyo imepita. Leo Vijana bado wanaotea kuingia nchi zilizoendelea. Nchi za
Magharibi. Maisha yalikuwa magumu enzi zile, bado magumu leo, miaka arobaini na
sita baada ya Uhuru. Lakini Wazungu wamefunga mipaka. Hawataki wageni. Enzi hizo
ilikuwa vile vile. Kupata
“kitabu”ilikuwa kazi; leo pia iko kazi. Kupata visa ilikuwa kazi; leo pia iko
kazi.
Miaka kumi na mitano
iliyopita mtindo uliibuka kwa Mwafrika kujifanya mkimbizi. Hiyo ziku hizi
imeshatafutiwa ufumbuzi. Wazungu washajua. Washajua mathalani kuwa Bongo hakuna
vita. Yalipokuja mauaji na machafuko ya Burundi na Rwanda wengi tukaanza na
sisi kujifanya wakimbizi kutoka sehemu hizo. Ujanja huo ulifaa hadi miaka
michache iliyopita. Leo yamegeuka. Wahusika washagundua. Ukimbizi leo haufai
tena kama sababu. Yuko jamaa kanieleza ujanja mpya. Kujifanya junya au firauni.
Si mnajua tena kuwa jadi hii nchi za Kizungu inaruhusiwa? Mwanaume kuoa
mwanaume au mwanamke kumwoa mwanamke mwenzako?
Mwezi jana ilipitishwa
sheria Uingereza kuwa ukishtakiwa kuwa umemtania msenge au firauni unakwenda
jela miaka Saba. Vituo mbalimbali vya polisi vina vitengo maalum vya kutetea
maslahi ya wasenge, na vinaongozwa pia na polisi wasenge. Basi kusikia hayo
walala hoi nao wamegundua mpya. Afrika tabia hii hairuhusiwi wala si mila yetu.
Basi ukitoka kwenu ukisema umeteswa kwa kuwa wewe msenge, ah unakaribishwa
mikono miwili. “Kwani watakucheki?” anauliza mpambe aliyenieleza. “Watakucheki
vipi? Watakufungua makalio?”
Basi, ndoto na njozi za
kutoka Afrika kwenda Majuu hazikuanza leo. Kitabu kipya cha Mzanzibari Shafi,
kitaonyesha harakati hizo miaka ya zamani kabla wengi hatukuzaliwa. “Mbali na
Nyumbani” anasema kimeshauliziwa na wachapishaji kadhaa hapa Bongo na Kenya.
Pichani chini Adam Shafi akinisomea muswaada.
Lakini swali niulize.
Wangapi wanamfahamu Adam Shafi? Kwa wasomaji wa vitabu vya hadithi na fasihi,
jina hili ni la kusisimua na kuvutia. Kwa wapenzi wa lugha yetu tukufu ya
Kiswahili huyu ni mjumbe. Walii. Tarishi. Al Watan. Mpiganiaji. Mbunge wa lugha
hii. Ndugu msomaji nikupe mfano? Hebu kumbuka Wabongo wangapi wanaodai eti
hawana msamiati wa kutosha
kujielezea Kiswahili.
Utamsikia mtu kasoma, ana shahada, ana ujuzi na utaalam wa hali ya juu akisema
: “Ah siwezi kuandika barua kwa Kiswahili…” Ilhali (lakini) anaongea Kiswahili
fasaha lakini kuandika anashindwa. Anatumia Kiingereza. Kiingereza chenyewe
marea nyingi kibovu. Afadhali hicho Kiingereza kingekuwa kizuri. Msikilize babu
na gwiji wa fasihi ya Kiswahili, Ustaadh Shaaban Robert akituasa katika Utenzi
wa Adili:
“…Lugha humpa hadhi
Kutumia ajuaye.”
Kisa cha kusema haya
yote nini?
Ukitaka kuboresha
lugha, ( yeyote ile) soma vitabu. Soma hadithi. Soma mashairi. Kama vile
ambavyo wanamuziki hujiendeleza kwa kusikiliza miziki ya aina mbalimbali,
msamiati, lahaja na lugha huendelezwa kwa kusoma vitabu. Kwako msomaji
unayegomba huwezi kujieleza vizuri kwa Kiswahili, au kuandika
Kiswahili…katafute vitabu vyake Adam Shafi,
utafaidika na kustareheka.
Watanzania tunasemwa
hatusomi. Baa ziko nyingi kuliko maduka ya vitabu na maktaba. Taifa lenye watu
wasiosoma linajichimbia kaburi la ujinga.
Nikiwa na Shafi, mjini
Milton Keynes alipopitia juma lililopita. Picha imepigwa na Hawa Yaxley.
Hebu onja (kidogo) baadhi
ya ubingwa wake wa matumizi ya lugha katika nukuu zifuatazo (hapa ni vitabu
viwili tu):
“Alihisi Shihab alikuwa
kama aliyemtupia mshipi akaumeza pamoja na ndoana, chambo na chubwi.” (Vuta
Nkuvute).
“Aziz alitaka kuibusu
midomo ya Khadija. Amemwinamia, uso umembadilika, uchu wa mwanamke umemtawala
akili zake zimehama kutoka kichwa cha juu zimehamia kichwa cha chini. Alipotaka
kumbusu Khadija alimtemea mate yakamtapakaa uso mzima. Alimwachia mkono mmoja
ili ajipanguse yale mate, Khadija
akaukamata mkono wake akaung’ata, Aziz akasikia maumivu makali yakipanda mpaka
utosini.” (Haini).
“Midomo aliitafuna
tafuna nakuimungunyua mungunyua kama mtafuna tambuu…” (Vuta Nkuvute).
“Tokea siku ile
aliposokomekwa ndani mle, furaha kwake ilikuwa adimu na huzidi kugubikwa na
majonzi pale anapowaza kwamba kosa alilolifanya ni kule kuchinja jogoo lake
mwenyewe…” (Haini)
“Amle Mbiza, amle
Mboza? Aliwaona kama wote wawili wamemsimamia mbele ya macho yake, achague
mmoja. Huyu mmoja keshaolewa, mke wa watu, amemfungia safari kutoka
Mombasa mpaka Unguja.
Akimwoa kitakuwa chuo chake cha pili. Huyu mwingine bado mbichi, mwari, bikira,
atakapomwoa itabidi arusi aijibishe mwenyewe. Arusi ijibu; yeye ajithibitishe
urijali wake na mwenzake athibitishe ubikira wake.” (Vuta Nkuvute).
Waandishi wengine:
Waandishi wengine:
0 comments:
Post a Comment