Mjomba'ngu Shamshi |
Kuzaliwa kwangu
kulifululizwa na majonzi yas’o kuwa na mfano. Hili si ada kwa wana wengi
duniani. Na kama ilivyokuwa kawaida katika jamii za kwetu Raha, waliniona
mwenye shari hivyo kunipa jina Tabu. Japo haya si kuyanga’mua papo kwa hapo,
niliyafahamu mtuo kwa mtuo kadri miaka ilivyozidi kuporomoka.
Usishangae kuwa haya
niliyapata kupitia kinywa cha Mjomba’ngu Shamshi, wala si kwa wavyele wangu. Bw
Shamshi alikuwa kabugia chumvi vya kutosha. Mvi zilimtambaa pote palipokosa
upara na masharubu yal’okosa kutiwa wembe yakimpa raha alo’zielewa mwenyewe.
Sina shaka kuwa hamna mwanamke mwenye tambo wala heba angetamani kumpa mkono
kwa madhumunni ya kumsabahi wala kumjulia hali...Umbo lake lilitisha!
“Hamna zima lis’o kuwa
na doa wala dosari. Hamna lenye dosari lisilokuwa na lake jema.” Hilo
nilijifunza kutoka kwa huyo mjomba’ngu. Matendo yake yalikuwa tofouti na sura
yake kwa kiwango kikubwa... Moyo mkunjufu tena ul’ofurika utu na fadhili.
Mshari na mwenye bidii ya mchwa.
“Tabu mwana’ngu”, aliniita
siku moja baada ya mchana kutwa kutupa kisogo kwenye kijishamba kidogo
alichokimiliki tangu zama za baba’ke. Sasa miaka yangu iliikuwa imeshavuka kuwa
ya mtu mzima eti. Mtu mzima gani na hata mlango wa darasa sijawahi kuujua?.
“Naam mjomba”,
nilijipenyeza kati ya moshi hadi alipokuwa kajipweteka ‘kochini’. Napaita
kochini mana’ke hapakuwa na pengine pa kupaita hivyo. Niliogopa sana pasi’je
wageni na kuliona hilo jiwe letu kisha ayatie majitapo yetu majaridani.
Sebuleni petu, ndipo palikuwa malazi petu pia. “Ndio Mjomba”, nilivunja kimya
chake baada ya kuketi mkekani mkabala na’ye.
“Chakula kimeshika moto?,”
“Nusu
saa hivi mjomba. Wajua tena mihogo huchukua m’da kuiva”, nilikejeli. “Tusubiri
tu.”
Kimya kilijipenyeza kwa
sekunde kadha. Labda kunipa fursa ya kujitoa nta masikioni. “Alivuta kohozi kisha
akanitupia macho. Macho ambayo kwa siku nyingi niliona soni kuyatazama.
“Leo naiona siku njema
kwetu kusemema na kusemezana yanayotuhusu katika maisha haya ya jua.” Alitua
kidogo, halafu, “N’na uhakika umekuwa na maswali chungu nzima tangu ulipouona
mwangaza wa dunia hii iliyosheheni madhila na karaha... Labda unadhani nilishi
‘ivi tangu zama za ujana wangu. Maisha ya ukapera pasi na wana wa uume wangu...
Siv’o, siv’o nilivyokuwa.”
Nilitamani atue kidogo
lakini hakukimya. Maneno ya mtima wake yaliyeyusha ujabali wangu. Nilihisi
michirizi ya machozi ikinishuka mashavuni. “Potelea mbali,” nilikubali
yanishuke hadi yatakaporidhika.
“Usidhani
ulitoka mbinguni. Ulikuwa na wazazi, tena wawili.”
“Lo! Mungu wangu we”,
moyo ulinipiga beni. Baridi yabisi ikanivaa ghafla. “Wako wapi wazazi wangu.
Mbona wanipe fursa ya kuonja uchungu wa ulimwengu na walimwengu huku wao
wapumua?, mbona hamna aliye nipasulia mbarika mapema? Kwa nini?, mbona”,
maswali yalizidi kuniduru kwa mfululizo. Majibu nayo?... labda alikuwa nayo
Mjomba.
“Zamani, eneo hili letu
lilitawaliwa na makundi haramu. Makundi ambayo kwa imani yao, walikuwa watetezi
wa haki za wal’odai kunyimwa hatimiliki za mashamba.” Alivuta pumzi ndefu kasha
akendelea, “serikali haikuwatadhmini hivyo. Kwayo, haya yalikuwa makundi yenye
dhana na nia mbovu.”“Halafu”, nilijikiza kusema ili
nisimnyime ulimi mjomba”
“Waume wote
walishurutishwa kujiunga na aidha mojawepo ya makundi hayo au kukatwa pumzi...
Hatukuwa na jingine. Vita kati yetu na wanajeshi vilishika kasi. Siku zilipita,
majuma yakatupa visogo, nayo miezi ikaipisha miaka. Wengi wetu walitiwa silili,
wengi wakazikwa wangali hai huku wengine wakitenganishwa na aila zao...”
“Baba’ngu na Mama’ngu
je?”, nilitamani kujua mara moja. Licha ya tamaa yangu, Mjomba alishikilia uzi
ule ule wa ‘hadithi’.
“Hatima’ye tulikusanya
virago vyetu na kujikokota hadi zizini.” Sauti yake ilikuwa sasa kati ya majonzi
na majuto. “Tulifa moyo!”, akaendelea, “Kwa bahati mbaya, Baba’ko mzee Majali
alikuwa miongoni mwa hao wal’otiwa pingu. Tulijaribu kadri ya uwezo wetu
kumwokoa bila mafanikio. Baada ya mwaka mmoja ‘ivi, tuliamkia habari kuwa
alikuwa amekata roho…”
“Eh!, wasema ba’ hayupo tena?”, niliuliza kwa
woga, jitimai na tamaa ya kujua zaidi ya’lomfika baba.
“Ndio
Tabu”, alinihakikishia kuwa sikuwa njozini bali katika uhalisia wa maisha.
Maisha ambayo kwangu yalikuwa ya shubiri tu. “Tulitarifiwa kuwa ukomo wake
ulisababishwa na mazoea yake ya ucheshi.”
“Mjomba”,
nilimkata kauli.
“Naam”
“Wasema
kauwawa na uchesi?”
“Hujakosea,
ndiv’o tulivyoelezwa” aliendelea, “ndani ya siri zetu tuliufahamu ukweli lakini
hamna angeliweza kuusema. Baba’ko walimwua wao tena kwa kumchoma moto…”
Nilielezwa mengi. Lililoniatua moyo
zaidi ni kuwa nina’ngu alinitoroka mara tu alipojifungua na kugundua kuwa
nilikuwa mlemavu. Ni kweli, mi’ ni mlemavu. Kibyongo ndi’vo wengine
walinitambulisha. Mama aliniona mwana wa nuksi kwake na kwa jamii.
Nilijihurumia kwa’lo, lakini ningefanya’je ilhali Jalali kaniumba ‘ivyo?.
Jingine ni kuwa Shangazi, yaani mkewe mjomba, alimtaliki kwa kisingizio kuwa
ye’ ni masikini. “Alitoroka na wana’ngu wawili na kwa ma’na hiyo, nikafanya
uamuzi wa kukulea wewe.”
Jinsi
umri ulizidi kumsakama Mjomba, ndivyo nilizidi kumhurumia zaidi ya
nilivyoihurumia nafsi yangu. Nguvu zilimpungua pole pole hadi ilipofika siku ya
kumtoka kabisa na uhai wake. Nazikumbuka dakika zake za mwisho alivyokuwa
sindano na nasaha zake. Uso ulijaa makunyanzi huku maneno yakimtoka kama
yal’olazimishwa. Alianza kuninasihi huku midomo yuamcheza, “Mwana’ngu siku
imenijia. Siku ambayo sharti ulimwengu wetu utengane.” Alijikaza kusema, “Yako
aifahamu mwumba wetu… Unakazi ya kufanya kwa aidha ufanisi wako au wa wenzako…
Usije ukakata tama kamwe!”
“Mmmh!,”
nafsi yangu ilitega sikio.
“Umasikini si tishio, almuradi unautajiri wa
siha njema.” Kwa ghafla, mawazo yangu yalizama kwengine. “Amenena kweli, ni
utajiri gani unaozidi afya, amani na imani?, wakwasi wangapi wanalia kila jua
lichomozapo?... ni wengi… ni wengi!. Nilijipa jawabu pasi na uhakika.”
“Umekuwa
chini ya mwavuli wangu kwa siku ayami. Umeshakomaa Tabu, umeshakua lakini
katika ulimwengu wa raha na karaha nd’o unaziliwa upya. Mchana jua
litakuangazia, usiku litajificha na hivyo kukwacha kwenye mataa ila naomba
ufahamu fika kuwa upo mwezi wenye uwezo wa kukupa mwangaza wa maisha wakati wa
kiza. Kulia na kuteremea ni damu moja. Leo utalia kesho utakenua. Leo
utatabasamu ‘alafu kesho utanuna na kufura mithili ya mahamri… Uamuzi unao
vitangani, leo yako nd’o kesho yako. Epuka umbea wa watu. Kuwa na utu bila
kutu… Jikaze!...”
Alikimya
tangu hapo. Akafa!.. Kimya cha daima.
Mwanzo niliona tofouti kubwa kuwa peke yangu
chini ya ‘kasri’ ambalo sasa lilikuwa langu.
Nilizidiwa
na shughuli za nyumbani na ‘izo za shamba. Labda hilo ndilo lililonitia motisha
ya kulitafuta jiko langu. Kwa hakika, sijawahijitosa katika lindi
hili, jinsi ya kuanza wala ya kuhitimisha sikuifahamu. Niliamkia vichochoroni kulisaka
kwa miezi kadha huku nikirejea mastakimuni mikono mitupu. Nilishuku kuwa
ulemavu wangu ulinipa mateso hayo ya kuambua nyayo na…
2012
swahilihup
swahilihup
this is perfect Click here for more news
ReplyDelete