Shamshi lenye uhai lilikuwa lishachomoza, ishara kuwa ilikuwa mwanzo wa siku njema kwani siku njema huonekana asubuhi. Ingekuwa siku ya kukata na shoka kwani sahibu wangu Yohana angeuasi ukapera kwa kufunga akidi za maisha na kidosho Rebeka, waliyekutana na kupendana tangu tulipokuwa chuoni. Niliharakisha kujitayarisha ili nielekee kule kwani chelewachelewa utamkuta mwana si wako.
Takribani mwendo wa saa nne na nusu, mambo yalikuwa yametengenea. Kanisa lilikuwa limepambwa likapambika. Maputo ya kila aina na kila rangi yaliangikwa na kutundishwa ukutani. Tungu za mle kanisani zilimwayamwaya mwangaza na kufanya mle ndani kuwa mchana zaidi.Pengine kanisa lingekuwa likipambwa vile kila Jumapili, lingewavutia na kuwanata waumini chungu nzima. Mimbarini, mandishi makubwa ya rangi tofauti yalionekana na kusomeka eti: ‘REBEKA AOLEWA NA JOHANA ’
Mara ghafla Yohana na kundi lake liliwasili. Waume na vijana waliovalia nadhifu walimfuata unyounyo. Yohana alionekana mtanashati ajabu. Nilimhusudu. Ungelimwona msomaji wangu siku hiyo, usingelijua kuwa ndiye kijana aliyekuwa akipata adhabu siku zote shuleni kwa kuvalia sare zilizochakaa na kujaa makunyanzi kana kwamba zimetafunwa na ng’ombe na kisha kutemwa. Nywele zake daima zilisokotana kama vidude vya vinyesi vya mbuzi. Lakini kumbe maisha humbadili mtu. Pengine ni mapenzi ndiyo humafanya mja kubadilika.
Sasa Yohana alivalia suti nyeusi ti! na tai ndefu juu ya shati lake jeupe. Ndevu zake alizoziacha zilimwongezea haiba iliyofanya wengi kumtamani. Akapokelewa kwa shangwe kuu na kuingizwa kanisani.
Muda mfupi baadaye liliwasili kundi la bi arusi, Rebeka Mapesa na wafuasi wake.
Waliwashangaza mno waumini kwa namna walivyong’aa. Rebeka mwenyewe alivalia nguo ndefu iliyomfunika hadi miguuni na kumpwayapwaya. Uso wake usingeuona kwani alikuwa kafunikwa kotekote. Sijui alionaje alikokuwa akikanyaga kwa kuwa mwendo wake ulikuwa wa mzofafa tena wa polepole kama kobe. Alikaribishwa na nyimbo za kuongoaongoa na kufuatilia zulia nyekundu waliyotandikiwa kuingia kanisani.
Kanisa lilijaa watu kutoka tabaka mbalimbali. Si wageni walioalikwa, si wazazi na watu wa jamii zote mbili na pia baadhi ya tuliosoma nao. Nyimbo ziliimbwa na masomo kutoka katika kitabu takatifu yakasomwa. Ikafika kilele. Wakati wa kuwaunganisha wawili hao. Kasisi aliyevalia mavazi meupe pe na nadhifu kana kwamba kukubaliana na ndoa yao alisonga mbele tayari kutenda kazi yake muhimu ya siku. Wawili wale wakawa wamesimama mbele yake. Kutoka nilikoketi, Rebeka alionekana malaika wa Mungu.
Wengi tulimmezea mate ndanindani lakini macho yake Yohana yalionekana kutuonya kuwa bahati ya mwenzio usiulalie mlango wazi. Aidha, nilikumbuka amri ya Mungu iliyoonya dhidi ya kutamani mali ya mtu mwingine.
“Kabla ya wawili hawa kuunganishwa na kufanywa kuwa kimoja, kuna yeyote aliye na pingamizi?” kimya kikuu kikaibia. Hakuna aliyejitokeza na swali likarudiwa mara mbili na kasisi. Kisha mwanaume mmoja aliyevalia nadhifu akanyanyuka kutoka kule alikoketi! Waumini nyoyo ziliwabapabapa na kuwaenda benibeni. Kila aliyeketi akawa ameachama, mdomo wazi kama pango la nyoka na kumtupia tazamo refu kama la mjusi. Mimi nilimjua kama Bohaz, kakake Yohana aliyesomea Ujerumani, akaishi na kufanya kazi huko. Alitaka tu kuhahikisha kuwa hakuna yeyote aliyepinga arusi ya nduguye. Ndio maana Yohana na mchumba wake hawakustushwa kamwe aliposimama. Lakini waumini hawakumjua ndio maana walishakata kauli mapema. Kumbe usilolijua ni kama usiku wa giza.
Ni wakati huo ndipo ilimjia msimamizi akilini kuwa pete zao zilisahaulika kule walikokuwa wakivalia na kufanyia mapambo ya Bi. Arusi. Alimnong’onezea kasisi mawili matatu na kuondoka kasi kama umeme. Kwa umbali kidogo, Yohana alionekana kukereketwa na kusinywa naye. Akatamani kumparamia na kumzabazaba makofi. Lakini alisimama patakatifu. Tena hakutaka kuonyesha hasira zake kwa umati. Pengine alikumbuka kuwa hasira hasara.
Wanakwaya wakaendelea kuwatumbuiza waumini na nyimbo za kikristo kwa furaha hata wakasahau kilichotokea. Wakadhihirisha bayana kuwa kuvunjika kwa mwiko sio mwisho wa mapishi. Waliendeleza nyimbo hadi msimamizi aliporejea muda si mrefu. Shughuli za awali zikaendelezwa. Maarusi wakakiri maneno baada ya kasisi na wakaanza kuvishana pete, huku kanisa zima limeja shangwe, vigelegele, hoihoi na nderemo pamoja na makofi ya furaha.
Kelele na furaha zilikatizwa ghafla na unyende kutoka nje. Mwanamke aliyeonekana chakaramu alikuwa akitimua mbio akielekea mimbarini. Alivaa nguo zilizoraruka na isitoshe alikuwa miguu mitupu.Maneno yalimtoka kwa sauti na haraka yasisikike vizuri. Vijitoto viwili vichafu vilimfuata pia mbiombio. Vilikuwa uchi na vilivyoparara ajabu! Mama yao alitamka kwa sauti kuwa Yohana alikuwa mumewe, baba ya vile vijototo. Eti walipendana na kuzaa vitoto hivyo kitambo kidogo Yohana alipokuwa angali chuoni! Kumbe ukistaajabu ya musa utayaona ya firauni.
Umati wa waumini uliduwaa na kuzuzuwaa. Kasisi bibilia ilimtoka mkononi na tang! Kuanguka sakafuni. Tayari vitoto vilianza kumpandiapandia Yohana na kumwitaita ‘baba.’ Yohana mwenyewe alipigwa na butwaa na akawa na mshtuko mkubwa. Parafujo za mwili wake ziliregea regerege na kukataa kumsimamisha imara. Rebeka alikuwa akifunzwa adabu na yule mwanamke chakaramu kwa kumwibia mume. Waumini wakajazana jukwani angalau kumwokoa. Nguo zake zilizokuwa nyeupe zilipata rangi mpya ya uwekundu. Mambo yalimwendea segemnenge na mvange, maji yakazidi unga na akazimia jukwani. Akawa amelala asijijue asijitambue. Jukwaa takatifu la Mungu likabadilishwa kuwa jukwaa la miereka na ndondi ya watu kupimana nguvu..
Naam, kilichoanza kwa mbwembwe na hanjam, sasa kilikuwa kikimalizika kwa fujo, rabsha, ghasia na vurumahi. Muumini mmoja alinivuta mabegani kwa nguvu akitaka kupita kuenda mbele kujionea sinema ya bure pia. Nikahisi uchungu wa ajabu na hapo ndipo niligituka na kupata kuwa misa ilikuwa imekwisha. Wanakwaya walikuwa wakiimba nyimbo za mwisho huku waumini wakiondoka na hapo ndipo mmoja alinigusa mbegani kuniamsha! Nilijinyanyua halahala kwa aibu hata sikutaka kuwatazama waumini walioonekana kunicheka. Kumbe nilikuwa nimelala muda huo wote kanisani mahubiri yalipokuwa yakiendelea na kupotelea katika ndoto hiyo! Niliapa kutoketi nyuma tena kila niingiapo kanisani kwa kuhofia kulala tena nyumbani mwa Bwana.
0 comments:
Post a Comment