Menyu

Swahili Hub

Hadithi


Wosia Wa Babu

Furaha iliyo’je kuwa kwenye kigonda changu  wakati kama huu wa magharibi?. Ha! Ha! Ha!... Siniulize mbona nimekenua ‘ivo, ipo siku katika umri huu wangu, utaijua sababu. Eti watamani kujua sasa ‘ivi?, aha! basi ni hivi, wapo wenye imani kuwa kuishi ni lazima almuradi keshazaliwa. Kubugia chumvi si sheria. Ni kwa kudura zake tu Rabana. Kupata dakika ‘izi za kusema nanyi wajukuu wangu, si kwa umri wangu, si kwa uwezo wangu, si kwa utajiri wala uchochole wangu. Ni majaliwa yake Jalali!.

Wazazi wangapi haswa akina baba wanaotenga angaa sekunde kadha kuwa na wana’o?, wangapi wanawanasihi watoto wao?... Jibu utakavyo ila fahamu ukweli upo wazi.
Oooooh!, nimekumbuka, hata sijawasabahi. Hujambo Hari?… vyema, sauti yako ina uvalana ndani yake. Sina shaka huwavutia sana wasichana kama huyu dada’ko Sabina. Sabina hujambo?... Shukran’ kwa kuzipokea salamu zangu. Kusudi la kuwaita hapa kwangu ni ili tuambizane yanayotuhusu. Pakiwa na lakuuliza, ni hapo baadaye.
Mwanzo naomba mtafakari juu ya maisha kwa jumla. Maisha ni ngazi. Maisha ni milima na mabonde. Maisha ni ndia telezi tena yenye ukavu wake. Kila mtu ana maisha yake lakini sote tuna hatima moja tena sawia. Wapo wenye mali na wajitambuao kama masikini, lakini juu ya yote, hamna tajiri wala masikini. Sote twala mwande kuchapo hadi jua  lituapo.
Mmmmh!, huenda hamnielewi vilivyo. Nitawapa kisa kimoja ili kuijenga taswira ya kitwndawili changu. Tangu nilipozaliwa na marehemu mama’ngu, nimeyaona na kujifunza mengi. Tulikokuwa tukiishi zama hizo, yaani Lodini, kuliwa kwa wakwasi tena wenye usemi. Familia yangu tu ndiyo il’otafsiriwa kuwa masikini kabisa. Ilipigiwa  mfano kote.
“Mama”, ungekisikia kijitoto kikimwambia mama’ke, “hiki chakula kimesalia nikipe mbwa au?”
“Mbwa?” angebwata, “leo wajifanyahujui eh!, tangu lini mbwa wakala matapishi kama hayo?, nenda kavitupe jaani. Wapo mbwa wenye njaa kuwazidi hawa wetu”… Eti waulizaje Sabina?... Mbwa gani wengine isipokuwa aila yangu?. Usitwae mwana’ngu.
            Tulijaribu kutoshirikiana nao kwa vyovyote vile lakini yote yalikwenda mvange. Si mwafahamu kuwa hamna mwenye njaa anayejitosheleza?. Licha ya kuwa kitinda mimba katika familia ya watu kumi na wawili, nilijitwika ya kuwalisha wakubwa wangu kwa kujishughulisha na uzegazega. Ulikuwa uamuzi ul’onitoa shuleni licha ya kuwa nilienzi sana elimu.
Nguvu za kukazana na ugumu wa hali tulimokuwemo, ziliwatoka wazazi wangu. Ndugu zangu wengine wakajihusisha na ulevi kwa kisingizia umasikini... [itaendelea]

            Haki zote zimenakiliwa na mwandishi
@dennis
2012

0 comments:

Post a Comment