Menyu

Swahili Hub

Malenga wa Mvita Ahmad Nassir


AHMAD NASSIR ni mzee mswahili wa Mombasa. Kwa upande wa babake ni Mtangana na kwa mamake ni Mkilindini. Hizi ni miongoni mwa kabila za asili ya Kiswahili za ki-mvita, yaani MombasaBwana Ahmad alizaliwa kuze, Mombasa mnamo 1936. Kama watoto wengine wa kimombasa wa wakati huo aliingia chuoni kusoma kuraani na dini ya kiislamu. Mafunzo hayo aliyapata kwa babu yake Sheikh Muhammad Ahmad Matano, mpaka alipohitimu.


Baada ya mafunzo hayo, alikwenda shule ya kizungu kwa wakati huo ikijulikana kama Arab Boys ( Serani Primary School) hapo hapo Mombasa. Kwa bahati mbaya hakumaliza masomo yake na aliwata (aliwacha) akiwa darasa la nne, na akaanza kufanya kazi.
Bwana huyu ni mshairi mashuhuri katika uwanda (uwanja) wa mashairi, anajulikana sana kwa jina la Ustadh Bhalo. Bhalo ni lakabu ya babu yake mzaa baba yaani juma Bhalo; na Ustadh ni cheo alichopawa na mhariri wa gazeti moja la Mombasa lilokuwa likiitwa SAUTI YA PWANI, baada ya kupata diploma yake ya ushairi.

KUTUNGA MASHAIRI
Lugha anayotumia Ahmad Nassir kutungia mashairi yake ni ile ya ki-Mvita, tena cha ndani. Kwa sababu hii, si rahisi kwa mtu mwenye ujuzi mdogo wa lugha ya Kiswahili kuyaelewa mashairi yake bila ya msaada. Mtu yoyote anayesoma mashairi yake akaona jinsi anavyoitezea (anavyochezea) lugha ataelewa kuwa Bwana huyu amekwasika na ni bingwa kweli.

Mpaka sasa ametunga mashairi mengi; na bado anaendelea kutunga. Baadhi ya mashiri hayo yamechapishwa na mengine bado. Kati ya mashairi yake pia yameimbwa na Mohamed Khamis Juma Bhalo al maaruf Professor Juma Bhalo katika nyimbo za taarabu, wawili hawa ni mtu na bin ammi yake.

Mashairi yake ya kwanza kuchapishwa ni yale yaliyomo katika kitabu kiitwacho` POEMS FROM KENYA’ kilicho pigwa chapa na The university of Wisconsin Press ya amerika katika mwaka wa 1966. Mashairi hayo yalifasiriwa kwa kiingereza na kuhaririwa na mwena zake Profesa Lyndon harries wa chuo kikuu cha Wisconsin. Kitabu cha pili cha mashairi yake ni kile kiitwacho MALENGA WA MVITA, hiki kimehaririwa na al marhum Shihabuddin Chiraghdin na kupigwa chapa na Oxford University Press, humu humu Kenya. Kitabu hicho ndicho kilichopokeya tuzo ya Kenyatta ya fasihi ya Kiswahili ya 1972 kuwa ni kitabu kizuri kuliko vyote vya Kiswahili vilivyotolewa mwaka huo. Vitabu vyake vyengine vilivyofwata baada ya Malenga wa Mvita ni; taa ya umalenga pamoja na Irshad.

Kuhusu mashairi yake ambayo hayajachapishwa ni mengi sana. Mbali na mashairi aliyonayo mwenyewe yako mengine kadha wa kadha yaliyo kwenye maktaba ya vyuo vikuu mbali mbali ulimwenguni kama German, Dar es salaam, London na hata Urusi.

Mbali na ubingwa wa mashairi pia ana kipawa cha uchoraji . miongoni mwa kazi zake za uchoraji ni zile zilizokuwa katika vifua za baadhi ya fulana za nyakati hizo za nyuma, kama zile za Cruel world,Cruel hand, please kiss me na make love not war.

Said A. Mohamed.

0 comments:

Post a Comment