Menyu

Swahili Hub

Elimu Kwenye Mtandao


Swahilihub

Na Mtemi Zombwe
KAMA inawezekana kwa bibi aliyeko kijijini kabisa kupokea fedha kwa njia ya mtandao kupitia simu yake ya mkononi,  vivyo hivyo inawezekana kabisa kwa mwanafunzi wa shule au chuo kusoma bila kuwa na karatasi  wala mwalimu. Ni teknolojia ya habari na mawasiliano iliyozaa elimu kwa njia ya mtandao.


Elimu kwa njia ya mtandao ina maana kuwa sasa  hatuhitaji tena kutumia muda mrefu kwenda mahali fulani ili kuhudhuria masomo; badala yake unaweza kupata masomo unapotaka, kwa muda unaotaka na  mahali popote iwe nyumbani, kazini, au katika maktaba iliyo karibu nawe.

Kwa wanafunzi wengi, mtandao  umefungua njia mpya na rahisi ya kuingia katika ulimwengu wa ujifunzaji ambao hapo awali ulikuwa umefungwa kwao kutokana na kukosa uwezo au mambo ya kifamilia. Na pengine ni kutokana na ukweli kwamba kozi walizotaka kusomea hazikuwepo katika maeneo yao isipokuwa ng’ambo nyingine ya ulimwengu.

Kwa maneno mengine, hakuna tena vipingamizi vya kijiografia katika kujifunza. Elimu kwa njia ya mtandao inasogeza mafunzo walipo watu, sio watu kwenda kwenye mafunzo.

 Kwa mfano, kama unataka kuhudhuria kipindi katika chuo kilichopo ughaibuni, sio lazima uende huko, unaweza ukatazama moja kwa moja katika intaneti, au ukiwa huna muda unaweza kutazama baadaye kipindi kilichorekodiwa.

Elimu kwa njia ya mtandao maana yake ujifunzaji sio tena wa hali ya kukaa tu, wanafunzi wote wameketi mbele ya mwalimu na “wanajifunza kwa kuelezewa”. Elimu kwa njia ya mtandao inafanya kujifunza kuwa zoezi la kivitendo.

Msisitizo wake upo kwenye uchangamano au “kujifunza kwa kutenda”. Hivyo, kwa mfano kama unataka kujua kuhusa kuchapa, unaweza kufanya hivyo kupitia ushirikishwaji kwa vitendo. Hutazami tu kuchapa ni jinsi gani bali unashiriki katika kufanya wewe mwenyewe.

Elimu kwa njia ya mtandao hufanya kujifunza kuwe kwa kusisimua, kushirikisha na kuvutia. Masomo magumu na ya kuchosha yanaweza kurahisishwa, kuwa ya kuvutia zaidi na kutamaniwa kupitia elimu kwa njia ya mtandao.

Hivyo, kwa mfano, kama tamthiliya ya Ngoswe Mapenzi Kitovu cha Uzembe,  haikusisimui, basi tazama moja kwa moja katika video, vitendo na vionjo vya mtendaji vinafanya usisimuke zaidi.

Ujifunzaji ni kazi ya kijamii, na elimu kwa njia ya mtandao inamaanisha kwamba ule uzoefu wa ujifunzaji madhubuti na wa kudumu unaweza kufikiwa, sio tu kwa kupitia maudhui, bali kupitia mitandao ya kijamii ya moja kwa moja katika intaneti.

Hapa wanafunzi wanahamasishwa kuwasiliana, kushirikiana na kushirikishana maarifa. Kwa njia hii, elimu kwa njia ya mtandao inasaidia “kujifunza kibunifu na mjadala changamfu”.

Elimu kwa njia ya mtandao inawezesha wanafunzi kumudu mafunzo yao na kwa njia sahihi kwa kila mwanafunzi. Sisi sote hujifunza kwa njia tofauti za kusoma, kutazama, kuchunguza, kutafiti, kuchangamana, kutenda, kuwasiliana, kushirikiana, kujadili, kushirikishana maarifa na uzoefu.  Elimu kwa njia ya mtandao maana yake wanafunzi wanaweza kupata fursa kufikia wigo mpana wa rasilimali za kujifunzia.

Elimu kwa njia ya mtandao pia inasaidia kuhusisha mafunzo ya ndani wakati wa kazi, kwa kuwa mashirika mengi yameanza kutambua kwamba kusoma au kujifunza si jambo linalofanyika darasani tu.

Kiuhalisi, asilimia  70  ya kujifunza huja wakati mtu yupo kwenye kazi ambayo sio mafunzo au elimu rasmi,  bali katika maisha ya kazi za kila siku kama vile kutafuta taarifa, kusoma nyaraka, kuzungumza na wenzao na mengineyo.

Ni aina hii ya kujifunza kusiko rasmi mbako elimu kwa njia ya mtandao inaweza kusaidia na kuhamasisha ndani ya shirika. Hivyo, kama wafanyakazi wanahitaji ufumbuzi wa matatizo wa haraka, hawataki kulazimika kujiandikisha kwenye kozi ya majuma kadhaa yajayo, wanataka majibu sasa hivi na kwa haraka. Hivyo, ufumbuzi rahisi na wa papo hapo ni kusoma  kwa njia ya mtandao.

Ujifunzaji umehama kutoka kwenye chumba cha darasa hadi kwenye kompyuta; na sasa kwenye simu za mkononi. Ni uhalisia kwamba wote tunakuwa watembeaji. Kwa mfano,  karibu asilimia 50 ya waajiriwa wote wanatumia hadi asilimia 50  ya muda wao wakiwa nje ya ofisi.

Sote tumekuwa wasafiri iwe kwenye daladala, gari binafsi, kwenye treni na ndege.  Kuna ushahidi wa kutosha kuonyesha kwamba watu wangependa kutumia vizuri zaidi muda huu muhimu katika mambo ya kujifunza.

Hizi ni baadhi tu ya sababu za  elimu kwa njia ya mtandao kuendelea kuwa muhimu zaidi. Lakini ili kunufaika na elimu kwa njia ya mtandao ni lazima utake kunufaika.

Tujibidiishe kupata ujuzi wa kompyuta na intaneti. Hizi ni fursa za kujifunza, kufanya biashara na kuendesha mashirika na taasisi kwa urahisi na ufanisi mkubwa. Tuzichangamkie!

[Kutoka Gazeti la Mwananchi.]

<<<




0 comments:

Post a Comment