Menyu

Swahili Hub

Vijana Katika Maisha ya Ndoa


Kwa heshima na taadhima nachukua nafasi hii kukukaribisha mpenzi msikilizaji katika makala ya vijana kutoka viunga vya Radio Vatican. Bila shaka utakumbuka kuwa majuma machache yaliyopita tulitafakari suala la wito kwa wanadamu wote kuwa watakatifu (Rejea, Walawi 19) na namna mbalimbali za kuishi wito huo zikiwa ni pamoja na ndoa, ukasisi na kujiweka wakfu kama mtawa wa kiume au wa kike. Leo, napenda kuufungua moyo na mawazo yako kuitazama nafasi ya ndoa katika jamii na hali za familia kwenye dunia ya utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.


Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanatufundisha kuwa ubora wa maisha ya mtu binafsi na jamii yote unategemea sana upendo uliopo kati ya mume na mke; na unategemea pia hali ya familia tunamoishi na mahusiano kati ya wanafamilia (Rejea, Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, Kanisa katika dunia ya sasa,GS, n. 47). Kama unavyoona mwenyewe, iwapo ubora wa maisha ya kila siku na ubora wa maisha ya dunia nzima yanategemea hali za ndoa na familia, kumbe, wanandoa na wanafamilia wote mnajukumu kubwa katika kuleta amani duniani, kuboresha maisha ya kila siku, wakijitahidi kujenga pia misingi ya upatanisho na haki.

SUALA LA NDOA

Katika suala la ndoa ni wazi kuwa, sio wote walioitwa katika wito huo, hata hivyo sisi sote, mimi na wewe ni wanafamilia. Haidhuru hali ya familia yako ipo namna gani!, lakini, tambua kwamba, kwa uwepo wako hapa duniani unapitia mikononi mwa familia, kwa maana pana ya kifamilia.

Kuna watu wengi wanaotumia nguvu zao, muda wao, kwa sala na majitoleo ili kudumisha ndoa na kuboresha familia zao. Nakupa pongezi kubwa wewe unayejitahidi katika hilo. Sitataja majina bali mnajifahamu, na hata wengine ni marafiki tunaofahamiana siku nyingi. Nawaomba sana, muendelee na moyo huo wa kudumu katika kuziboresha ndoa na familia zenu, katika nyanja mbalimbali. Nami nawaombea kila siku baraka na neema za Mwenyezi Mungu ili mzidi kudumu katika hilo.

Huwezi kufumbia macho baadhi ya mapungufu yaliyopo katika suala zima kuhusu ndoa na familia, na hii sio Afrika peke yake bali sehemu mbalimbali duniani. Bado kuna jamii zinazoendekeza mitaala, talaka, mapenzi kabla ya ndoa na uchumba sugu! Baadhi ya wanandoa wanaelemewa na ubinafsi zaidi dhidi ya wenzi wao, tamaa kupindukia na starehe kupita kiasi, utumiaji wa tendo la ndoa kinyume na taratibu zake, matumizi ya kinga zisizo halali. Bila kusahau jinsi ndoa na familia zinavyoyumbishwa na kukosa msimamo hata kuingia katika matatizo makubwa sababu ya hali za kiuchumi, kijamii, kisiasa na kisaikolojia.

Kufuatia mapungufu yote haya niliyoyataja hapo awali, vijana wengi leo wanatawaliwa na woga mkubwa kufunga ndoa na kuwa na familia. Sikulaumu swahiba wangu, ni kawaida kuwa na woga unapogubikwa na matatizo na hali zisizo na uhakika zinazokuzunguka.

Hata hivyo nakuomba ukumbuke nini tuliongea tulipokuwa tukijadili kuhusu kuota ndoto za kweli, kwa ujasiri, kwa matumaini, kwa sala na umoja ndani ya Fumbo la Utatu Mtakatifu. Mwenyezi Mungu yu pamoja nawe. Yeye ndiye chanzo na sababu ya utimilifu wa ndoa na familia, naye anakuongoza na kukulinda. Jiweke mikononi mwake na atakupitisha salama. Piga moyo konde na uwe kama Mzaburi asemavyo “Nijapopita katika bonde la kivuli cha mauti sitaogopa mabaya, kwa maana wewe upo pamoja nami, gongo lako na fimbo yako vyanifariji” (Rejea, Zaburi 23, 4).

Pamoja na magumu na dhoruba zote zinazoisonga ndoa na familia bado tunu hizi zinang’ara kati ya watu wengi wamchao Mungu na wanaoweka tumaini lao kwake huku wakiwajibika kikamilifu. Maana na uhalisia wa ndoa bado unalindwa. Heshima, ukuu na utakatifu wa ndoa na familia bado vinapeperusha bendera yake sehemu mbalimbali duniani.

Kutokana na hali hii duniani, Kanisa bado linatia nguvu-kazi katika mafundisho ya ndoa na familia na kuwatia moyo vijana kuendelea kuzienzi tunu hizi. Kwa majuma kadhaa kuanzia leo, pamoja na mambo mengine, utapata dondoo za kutosha kuhusu suala zima la ndoa na familia kutoka katika makala yetu ya vijana.

Tusipigane chenga juma lijalo, ntakuwepo hapa nikikusubiri ili tuendelee kubadirishana mawazo kuhusu maisha yetu ya ukristo, na kwa namna ya pekee jinsi ya kusonga mbele kama jeshi la vijana ndani ya Kristo, tukidumu katika imani. kwa ulaini kabisa nateleza namna hiyo kutoka viunga vya Radio Vatican, ni sauti ya kinabii, Celestin Nyanda.

<<<

0 comments:

Post a Comment