Yuko ambaye hajui na hajui kuwa hajui. Huyu ni banadamu ambaye kwake hakuna anachokijua hata kidogo, lakini siyo kwa kosa lake ila bado hajajuzwa juu ya mambo. Kwa jina la karibu twaweza kumwita Mjinga. Ujinga siyo tusi ila tafsiri yake ni mtu yeyote ambaye hafahamu wala hajui chochote. Kwa mfano, wewe kama hujui kitu chochote basi ni mjinga na ukumbuke kuwa ujinga siyo tusi. Lakini pamoja na hayo yote, binadamu wa sampuli hii, huwa hasemi asiyoyajua. Mintaarafu, ukikutana na binadamu wa namna hii ujue kuwa ni mjinga na anahitaji msaada ili kuyajua mambo. Mjinga!!!
Yuko ambaye hajui na anajua kuwa hajui. Huyu ni miongoni mwa binadamu ambao hawajitambui na ambao wanahitaji msaada wa hali ya juu. Sampuli hii ya binadamu, huwa hajui kitu chochote, lakini ni tofauti na mjinga ingawa naye ni mjinga. Ni mjinga kwa kuwa kama nilivyotangulia kusema kuwa ujinga siyo tusi ila kutojua jambo ambapo hata wewe ni mjinga katika jambo lolote usilolijua. Ila huyu ana nafuu kwa sababu anajua kuwa hajui. Hivyo ukikutana na binadamu wa namna hii huna budi kumsaidia. Msaidie!!!
Yuko ambaye anajua lakini hajui kuwa anajua. Hii ni miongoni mwa sampuli za binadamu zinazohitaji kukumbushwa. Binadamu wa sampuli hii anajua mambo, tofauti za sampuli zilizotangulia ila ubaya wa binadamu huyu ni kwamba yeye mwenyewe hajui kuwa anajua. Utamwona mathalani ana kipaji cha hali ya juu katika mambo fulani, lakini mwenyewe hafanyi jitihada za kukiendeleza kipaji hicho. Hii inatokana na kutojua kuwa ana kipaji cha namna hiyo. Ukikutana na binadamu huyu, huna budi kumkumbusha kwani hawapotei, ukimwona tu utamjua. Mkumbushe!!!
Yuko ambaye hajui na anajua kuwa hajui lakini hataki kujua. Huyu ni hatari kwa maisha yake mwenyewe na ukoo wake wote. Jambo hili humfanya ashindwe kujifunza kwa sababu huona aibu kujidhihirisha mbele za watu kuwa hajui, labda kwa kuhofia kuchekwa ama kubezwa. Kifupi hakuna binadamu aliyezaliwa anajua, ila ni jitihada za binadamu mwenyewe ndizo humfanya ama awe anajua au hajui. Binadamu wa sampuli hii wapo wengi na ukikutana nae huangalia pembeni na mara nyingine hujificha. Kibri!!!
Yuko ambaye anajua na anajua kuwa anajua. Binadamu wa sampuli hii ni mwerevu. Ni mwerevu kwa sababu anajua mambo, lakini siyo tu anaishia katika kujua mambo la! Anajua mambo, pia anajua kuwa anajua mambo, hivyo huwa rahisi kwake kufanya mambo kwa ujuzi na maarifa kulingana na jambo husika. Binadamu wa sampuli hii huwa na kawaida ya kujifunza na kudadisi mambo kwa kutumia mbinu mbalimbali hata kuna wakati mwingine huitwaWalaghai kutokana na kaida zao za kutaka kujua mambo. Mwerevu!!!
Yuko ambaye anajua lakini hataki wengine wajue. Binadamu huyu ni mbaya sana, tena sana zaidi ya UKOMA. Wana uwezo mkubwa sana wa kung’amua mambo na mbongo zao ni nyepesi katika kunasa na kufikiri juu ya mambo kadha wa kadha. Lakini binadamu huyu pamoja na kubarikiwa uwezo huo na Maulana, lakini ni mbinafsi kwani hataki kuwajuza wengine kile anachokijua na anachukia pale mtu mwingine anapojua anachokijua yeye.Mchoyo!!!
Yuko ambaye hajui, lakini anataka kujua. Binadamu huyu ni mjinga kwa sababu tu hajui, lakini pamoja ya kuwa ni mjinga ila huwa na kaida fulani hivi za udadisi wa kutaka kujua mambo. Anapohisi kuwa jambo fulani halijui, basi hakurupuki ila hudadisi kwa lengo la kulifahamu hilo jambo. Ni miongoni mwa tabia yake ya kudadisi ama kuuliza uliza jambo kama halijui na hataki kupitwa na jambo. Pamoja na kutaka kujua mambo, lakini mara nyingine hutaka kujua hata yasiyomuhusu, hii hutokana na tabia yake ya udadisi. Mdadisi!!!
Yuko ambaye anajua na anataka wengine wajue. Ukimwona binadamu wa sampuli hii, usikubali akupite vivi hivi. Kwa sababu wako wachache wenye tabia kama hii. Jambo zuri kwa binadamu huyu ni kwamba, pamoja na kuwa wako wachache, lakini hufanya jitihada mbalimbali kuhakikisha kuwa kila mtu anakijua kile anachokijua yeye. Ukikutana na binadamu huyu, hasiti kukuelekeza juu ya jambo fulani ambalo kama utalifanyia kazi basi manufaa chanya yatakuwa ni zao kubwa la maelekezo yake. Siyo Mchoyo!!!
Yuko ambaye hajui, lakini anajifanya anajua. Huyu ni zaidi ya UKOMA. Mara nyingi binadamu huyu hakuna anachokijua, lakini ajabu iliyoje, hataki kuonekana hajui, hataki kushindwa na jambo. Kwa hiyo anajitia ana ufahamu wa mambo kumbe wapi! Hana lolote. Binadamu huyu kutokana na tabia yake hiyo, basi hujikuta hana subira wala simile, akikuta binadamu wengine katika mazungumzo, atajitia kujua kila kitu kinachojadiliwa. Fauka wa hayo, hapendi kukosolewa wala hataki kupingwa. Pia ni mbishi huyo ajabu! Ukikutana na binadamu wa sampuli hii, wala usijishughulishe naye kwani atakupotezea muda wako bure. Mwache!!!
Yuko ambaye anajua, lakini hataki kujulikana kuwa anajua. Binadamu huyu hana hulka ya kutaka kufahamika kwa kile anachokijua. Mara nyingi binadamu huyu huwa kimya kama atafakariye jambo fulani na ukimwona utadhani kuwa hajui mambo kutokana na tabia yake ya kuwa kimya na kutopenda kujulikana na binadamu wengine. Utamwona amekaa peke yake na endapo utabahatika kumwona amekaa na binadamu wengine, basi huwa na hadhari kubwa ili asibainike kuwa anajua mambo. Pia huwa makini sana katika kuzungumza huku akiepa kutoa siri aliyonayo. Unaweza kuishi naye na usijue kuwa anajua. Msiri!!!
Yuko ambaye anajua na anataka kila mtu ajue kuwa anajua. Mwogope binadamu wa namna hii tena ukimwona jitahidi umpitie mbali kwani hana tofauti na dume la Nyani kwa tabia yake hii. Dume la Nyani lina tabia moja kwamba pale linapofika mahali, basi linataka kila kiumbe kilichopo mahala hapo kitambue uwepo wake. Ndiyo sampuli ya binadamu huyu. Ukweli ni kwamba anajua mambo, lakini tabia yake ya kujionesha onesha na kujikweza kila sehemu hata pasipostahili kufanya hivyo ndiyo kikwazo kwake. Akitoa msaada, basi mtaa mzima utahabarika na akifika sehemu basi yeye tu ndiye mwongeaji hakuna mwingine.Mbinafsi!!!
Eeeenhe!!! Hivyo ndivyo binadamu alivyo. Mwangalie huyo jirani yako, yukoje? Na wewe je, ukoje???
http://deniceshonko.blogspot.com/2012/07/ubora-wa-maisha-ya-binadamu.html
http://deniceshonko.blogspot.com/2012/07/utangulizi-1.html
http://deniceshonko.blogspot.com/2012/07/ubora-wa-maisha-ya-binadamu.html
http://deniceshonko.blogspot.com/2012/07/utangulizi-1.html
0 comments:
Post a Comment