Menyu

Swahili Hub

Riwaya ya Nyongo Mkalia Ini


UTANGULIZI

Tukichunguza hazina ya uhakiki uliofanywa katika taaluma ya fasihi ya Kiswahili na kuiweka katika mizani, upande mmoja ubebe tahakiki zilizozingatia maudhui na mwingine zile zilizoangaza fani, upande wa maudhui utalemewa na uzito na kuanguka. Ni kweli kuwa umuhimu wa fasihi katika jamii unatokana na jinsi ambavyo inaimulika jamii na kuichora kwa madhumuni ya kuihakiki na 


kuirekebisha kutokana na udhati na uzito wa mafunzo mwafaka inayoyabeba. Ni
kweli vile vile kuwa fasihi ni sanaa kutokana na matumizi ya pekee ya lugha na
vipengele vingine vya fani ambavyo kwa pamoja huipa sura maalum na kuyafanya
maudhui yake yatufikie katika hali na umbo linalovutia. Hali hii ndiyo huiwezesha
fasihi kutuingia, ikatuchoma na kutufikirisha zaidi. Ndio nguzo ya utamu wa fasihi.
Katika misingi hiyo, uendelezaji wa fasihi; hasa kwa upande wa uhakiki
unapaswa kuzingatia pande zote mbili  za sarafu; yaani maudhui na fani
inayoyabeba maudhui hayo. Makala hii imelengwa kutoa mchango huo kwa kuupa
uzito upande wa fani ya fasihi kwa kuzingatia kipengele cha usimulizi. Nao uteuzi
wa usimulizi umechochewa na ukweli kuwa mbinu hii haijachunguzwa na wahakiki
wengi katika fasihi ya Kiswahili. Awali ya kuchambua jinsi ambavyo mbinu hii ya
usimulizi imejitokeza katika riwaya ya Nyongo Mkalia Ini, dhana ya usimulizi
itafafanuliwa na nafasi yake katika fasihi kuwekwa bayana.

1. DHANA YA USIMULIZI 
Katika masimulizi ya ngano, msimulizi ama fanani alijidhihirisha wazi wazi mbele
ya hadhira yake. Kwa hivyo, kulikuwa na uhusiano, pamoja na mawasiliano ya
moja kwa moja kati ya msimulizi na hadhira yake. Fanani aliweza hata
kuwashirikisha wasikilizaji wake kwa kuwauliza maswali au hata kuwaimbisha
sehemu za nyimbo zilizotumika katika masimulizi ya ngano. Hadhira nayo ilishiriki
kwa kuitikia, kushangaa, au kusinzia, yote ambayo yalitoa ishara maalum kwa
msimulizi.

Baada ya uvumbuzi wa maandishi kazi nyingi za fasihi zinapatikana katika
maandishi na hivyo usimulizi dhahiri haujitokezi katika kazi hizo. Tunayategemea
maandishi kuupata ujumbe wa wasanii ambao wakati mwingi hatuwafahamu. Ni
wazi kwamba sifa nyingi ambazo zilipatikana katika uhusiano wa mtambaji na
49 Nordic Journal of African Studies

hadhira yake haziwezekani hivi sasa, lakini bado swala la usimulizi ni la kimsingi
sana katika uwasilishaji wa kazi mbalimbali za fasihi, hasa za nathari. Hatukosi
kuisikia sauti ya msimulizi angalau katika akili zetu iwapo si katika masikio yetu
pale tunapoifuatilia hadithi kwa kuisoma.

Kulingana na Attenbernd na Lewis (1963), usimulizi ni ule mkabala ambao
hutuwezesha kuyatizama yanayotendeka na kusikia yanayozungumzwa katika kazi
ya fasihi. Mlacha (1991), anauona usimulizi kama uhusiano uliopo baina ya
msimulizi na hadithi yenyewe. Namna ambavyo msimulizi anaingiliana na hadithi,
na nafasi yake katika uwasilishaji wa hadithi ndiyo hutuelekeza kufahamu usimulizi
wake. Njia nzuri ya kuelewa hali hii ni kutambua ni nani anayetuwezesha kuipokea
hadithi yenyewe; yaani matukio mbalimbali yanawasilishwa kwetu kwa kupitia
kwa macho ya nani? Kimsingi, kuna maswali kadhaa ambayo huiweka wazi zaidi
mbinu iliyotumika katika usimulizi. Ni vizuri kuelewa ni nani anayeisimulia kazi
hiyo na ana mtazamo gani? Ana uhusiano gani na matukio ya hadithi husika?
Jambo la muhimu katika swali hili ni uelewaji wa uhusika wa msimulizi. Anashiriki
katika hayo matukio au la? Ni muhimu vile vile kuchunguza kama mtazamo wake
wa matukio hayo ni wa kuaminika. Hayo ni baadhi tu ya maswala muhimu ambayo
humsaidia msomaji wa kazi hiyo kuelewa msimulizi wake pamoja na mchango
wake katika kuikamilisha.

2. MBINU ZA USIMULIZI
Kuna mbinu nyingi za usimulizi ambazo mwandishi anaweza kuzitumia
kuiwasilisha kazi yake katika maandishi. Aina hizo za usimulizi hutofautiana kwa
jinsi ambavyo zinazua athari tofauti  kwa wasomaji. Kuna baadhi ambazo
hutuongoza kumulika hisia zetu kwa msimulizi ilhali zingine hutuashiria kuangaza
nadhari yetu kwa kile kinachosimuliwa. Kwa hivyo, mwandishi hupaswa kufanya
uteuzi wa mbinu mwafaka ya usimulizi atakayoitumia kwa kutegemea yale
anayonuia kuyasisitiza katika kazi yake.

2.1 USIMULIZI MAIZI
Msimulizi maizi pia huitwa msimulizi mwakote. Hawthorn (1985) anasema kuwa
huenda mbinu hii ilikuwa tokeo la mojawapo ya sifa za Mungu ya kujua kila kitu.
Mbinu hii ya usimulizi ndiyo kongwe zaidi kuliko mbinu nyingine za usimulizi.
Tukikumbuka kuwa katika masimulizi ya ngano msimulizi alielewa kila kitu na
hasa tabia zote za wahusika; inakuwa rahisi kuelewa ni kwa nini mbinu hii ni
kongwe zaidi. Katika mbinu hii mwandishi huieleza hadithi ambayo, mara nyingi,
yeye haimhusu; yaani haishiriki lakini, akiwa muumbi wake, anaelewa kila kitu
kinachotendeka hadithini.

50Usimulizi wa Riwaya ya Nyongo Mkalia Ini
Msimulizi anakuwa na uhuru mwingi sana. Anajua kila kitu na ana nafasi ya
kuamua yale atakayotuambia na yale atakayoyaacha. Ana uwezo wa kutamba na
kueleza maswala mbalimbali; na usimulizi unaweza kutumia mhusika mmoja,
halafu mwandishi akabadilisha na kutumia mhusika mwingine. Katika usimulizi
huu, mwandishi ana uhuru kiasi kwamba tunamtarajia kuelewa hata mawazo ya
wahusika wake. Kwa hivyo, msimulizi  huingia katika akili ya mhusika na
akatufafanulia mawazo yake, akatueleza hata kile ambacho mhusika
anakikumbuka, na pia msimamo wake kuhusu maswala mbalimbali.
Kuna baadhi ya waandishi ambao wanaitumia mbinu hii kwa namna tofauti
kidogo, na badala ya kutueleza tu  mambo kuhusu hadithi , wanadokeza pia
msimamo wao. Katika hali  hii, mwandishi anaeleza mawazo au msimamo wa
mhusika, anachanganua matendo yake na hata kufafanua wazi wazi kinachoyazua
matendo hayo. Zaidi ya hayo, anaweza hata kutoa tathmini ya wahusika wake kwa
kufafanua hulka zao (Attenbernd na Lewis 1963; Carpenter na Neumeyer 1974).
Kutokana na uhuru wake, mwandishi anaweza kutoa maelezo yote na kuingiza
mambo mapya bila lazima ya kueleza jinsi alivyoyapata. Uelewaji wa kazi hiyo
kwa upande wa wasomaji huwa umerahisishwa kwani msimulizi atatamba kote
kule hadithi inatukia na kuyaweka wazi matukio yote. Mwandishi anapotumia
mfumo tulioutaja wa kutoa msimamo wake mara kwa mara anakumbusha wasomaji
kuwa ndiye ameibuni na wala wayasomayo si matukio ya kikweli; hasa iwapo
wanamfahamu mwandishi mwenyewe. Kwa upande mwingine, matukio
yanaposimuliwa bila kutolewa maelezo na mwandishi, kuna uwezekano mkubwa
sana wa wasomaji kutekwa na matukio hayo yanayojipambanua yenyewe bila
kumkumbuka mwandishi. Mbinu ya msimulizi kutoa msimamo wake kuwahusu
wahusika au matendo yao (“editorial omniscience”) inamfanya aingilie kati badala
ya kuwaachia wasomaji nafasi ya kutafakari na kujiamulia wenyewe.

2.2 USIMULIZI WA NAFSI YA TATU
Katika usimulizi huu mwandishi anasimulia akitumia nafsi ya tatu lakini anajikita
zaidi katika mhusika mmoja tu. Anajibana na kujipunguzia anayoyafahamu kwa
kudhihirisha ufahamu wa mhusika mmoja peke yake. Yote anayoyajua ni kumhusu
huyo mhusika na haonyeshi kuwafahamu wahusika wake wengine. Kwa hivyo,
mawazo, mwelekeo na msimamo wa mhusika huyo mmoja ndio mwandishi
anaoutambua kwa undani. Hapa mwandishi huwa amejipunguzia uhuru wake wa
kuyaeleza yote anayoyajua kuihusu hadithi yake. Mhusika anayepewa nafasi hiyo
aweza kuwa mhusika mkuu au mhusika mwingine yeyote hadithini.
Kulingana na S. A. Mohamed (1995) usimulizi wa nafsi ya tatu ni ule
unaompatia mhusika mmoja nafasi ya kusimulia hadithi badala ya msimulizi
mwakote kuisimulia yote. Ametoa mfano wa bwana Msa wa Mohamed S. Abdalla
(1976) ambaye hupewa wakati kuendeleza masimulizi ya hadithi na kusimamia
mawazo ya mwandishi. Jambo muhimu linaloibuka kutokana na mawazo ya
51Nordic Journal of African Studies
Mohamed ni kuwa mbinu za masimulizi zaweza kuchanganywa katika kazi moja ya
fasihi.

2.3 USIMULIZI WA NAFSI YA KWANZA
Katika mbinu hii ya usimulizi mwandishi hupotelea ndani ya mmoja wa wahusika
wake ambaye husimulia hadithi yote. Mohamed (1995) anasema kuwa mbinu hii si
rahisi kama inavyoonekana kwani mwandishi anapaswa kuwa makini asitumie ‘ni’
na ‘mimi’ kwa wingi hadi akawachosha wasomaji wake. Japo mbinu hii
haijatumika sana katika fasihi ya Kiswahili, kuna mifano ya hapa na pale.
Msokile (1981) ana hadithi ya “Roho Nyeusi” inayoanza hivi:
Nayainua macho yangu kwa mara nyingine na kumwangalia Beata kwa hasira
huku kimoyo chake kitete kikidunda taratibu kifuani pake¼(uk. 49)
Aidha, Ruhumbika, katika hadithi ya “Wali wa Ndevu”, Parapanda, anatumia
mbinu hii:

¼Si nia yangu kusimulia tena maajabu tuliyoyaona visiwani, majumba malidadi
ajabu ya kukaa , bure, wananchi, mabarabara safi ya kisasa¼.(uk. 63)
Mifano hiyo miwili inadhihirisha kuwa masimulizi katika hadithi hizo yanafanywa
katika nafsi ya kwanza. Mbinu hii inawasilisha hadithi kama ambayo imesimuliwa
na mmoja wa wahusika wake. Kunakuwa na matumizi ya ‘ni’; kiwakilishi nafsi ya
kwanza. Mhusika anaweza kuwa nguli (“Roho Nyeusi”) ambaye anasimulia hadithi
yake mwenyewe, ama akawa mhusika mdogo tu akieleza yaliyomkumba nguli.
Kwa mfano, katika “Wali wa Ndevu” msimulizi wake ni mhusika mdogo tu.
Usimulizi huu humbana sana mwandishi kwani kuna mambo mengi sana
ambayo hawezi akayaeleza bayana. Kwa  mfano, mawazo ya wahusika wake
wengine hayatatufikia vilivyo. Itaonekana kuwa katika hali hii tunalazimika
kutizama mambo kupitia kwa mtu mmoja, tunayemtegemea kutueleza mambo
ambayo hatuyashuhudii wenyewe. Mwandishi anaweza kuamua kutumia
mazungumzo baina ya wahusika, barua au mbinu nyingine ili kutupanulia mtazamo
wa kazi yake.

Carpenter na Neumeyer (1974: 184) wanatoa mawazo yafuatayo kuihusu mbinu 
hii: 
Wasomaji wanagenzi huweza wakachukulia kuwa msimulizi wa nafsi ya kwanza
ana mawazo sawa na ya mwandishi. Si lazima iwe hivyo na wakati mwingine
mawazo yake ni kinyume kabisa na yale ya mwandishi mwenyewe.
Kwa hivyo ni makosa kuyaoanisha mawazo ya msimulizi wa nafsi ya kwanza na
yale ya mwandishi kwani msimulizi kama huyo ni mhusika kama wale wengine
hadithini na wala si lazima awe msemaji wa mwandishi. Hata hivyo, mbinu hii ina
faida zake. Wakati mwingine mwandishi hutaka tuutizame ulimwengu wake kupitia
52Usimulizi wa Riwaya ya Nyongo Mkalia Ini
kwa mhusika maalum, kama vile kijana mdogo, mama mzee, na kadhalika.
Tuyaelewe maisha kupitia kwa mtazamo wa aina fulani ya wahusika. Kwa baadhi,
hadithi inayotumia usimulizi wa nafsi ya kwanza huwa hai zaidi kwani huifanya
hadithi ifanane na maisha ya kila siku.
Vile vile katika usimulizi huu mwandishi huficha mambo ambayo msimulizi
wake hayatambui mpaka pale ambapo yatahitajika katika maendeleo ya ploti, hasa
katika hadithi za upelelezi.


3. USIMULIZI WA NYONGO MKALIA INI
Kila hadithi ina mwandishi. Aidha, ina msimulizi ambaye yuaweza kuwa
mwandishi ama mtu mwingine ambaye mwandishi anamwelewa vilivyo (Mlacha
1991). Sehemu hii itatalii namna ambavyo mwandishi Rocha Chimerah (1995)
amesimulia hadithi yake. Rocha si mgeni katika uandishi wa Kiswahili. Kando na
riwaya hii, mwandishi huyu amechapisha vitabu kadhaa, vikiwemo; Kiswahili Past,
Present and Future Horizons, na Mnara Wawaka Moto. Ameshirikiana na
waandishi wengine kuandika vitabu mbalimbali. Aidha, Chimerah amechapisha
makala kadhaa kuhusu lugha na fasihi ya Kiswahili.
Akiwanukuu Leech na Short (Mlacha 1991) anasisitiza swala la umuhimu wa
kujenga uhusiano baina ya mwandishi na hadhira yake ili anayoyaeleza
yapambanuliwe na kueleweka vyema. Ni sharti mtunzi katika kuumba na
kuwasilisha kazi yake, awafikirie wasomaji wake pamoja na kuzingatia njia bora ya
kuwawezesha kuipokea hadithi yake. Hili huathiri uteuzi wake wa njia ya
usimulizi.

Hadithi hii ya Nyongo Mkalia Ini imesimuliwa zaidi kwa kuelemea katika mbinu
ya nafsi ya kwanza. Hii hapa mifano ya kudhihirisha hali hiyo.
Nilinyanyua uso wangu nikariaria huku na huku. Ndio mwanzo niwatambue
haswa wenzangu tuliomo sote humu chumbani... (uk. 1)
...ikiwa bado una shaka, maelezo yangu  ya mwisho ni kwamba hoteli hii i
katikati ya Baraste ya Makadara. (uk. 8)

Nikisema nilipata usingizi wa haja, nadanganya. (uk. 95)
Matumizi haya ya viwakilishi mbalimbali vya nafsi ya kwanza ni dhihirisho kuwa
riwaya hii inasimuliwa na mmoja wa wahusika wake katika nafsi ya kwanza.
Anavyoonya Mohamed (1995), mwandishi anapoteua kutumia mbinu hii anapaswa
kuwa makini sana ili asitumie hizo "ni" na "mimi" kiholela na kwa wingi kiasi cha
kuwachosha wasomaji wake. Kwa hivyo mbinu hii, kinyume na imani ya watu, si
rahisi kuitumia pasipo kukinai wasomaji.

Mbinu hii hupelekea waandishi kujaribu kutuelekeza kuona kuwa anayesimulia
hadithi ni mtu mwingine kabisa na wala siye. Hili wanalitekeleza kwa kujaribu
53Nordic Journal of African Studies

kujitenga na wasimulizi kwa kuwataja wahusika wasimulizi kwa majina. Hivyo,
msomaji anabaki kudhania tu kuwa mwandishi ndiye huyo mhusika. Katika hali hii,
mwandishi anatoa rai na maoni yake kama mmoja wa wahusika wa hadithi. Licha
ya hali hiyo ya waandishi kutaka kujitenga na msimulizi wa hadithi zao, ukweli ni
kuwa kutokana na hali kwamba hadithi  yenyewe ni utunzi wa waandishi,
tunapozifuatilia hadithi nzima yale matumizi ya nafsi ya kwanza, kinyume na
kututenganishia mwandishi na msimulizi, kama anavyodai Mlacha (1991: 60),
yanatuongoza zaidi kutizama hadithi hiyo  kama inayosimuliwa na mwandishi
mwenyewe. Swala la mhusika msimulizi  kupewa jina tofauti na la mwandishi
halitufungi macho kwa sababu tunaelewa kuwa mwandishi ana uhuru wa kutumia
majina ya kubuni huku akirejelea mambo mahsusi. Vivyo hivyo, yuaweza
kujibandika jina la kisanaa.

Kutona na utata huo, mawazo ya Carpenter na Neumeyer (1974: 184) kuhusu
mbinu hii ni mwafaka sana. Wanaonya kuwa ni sharti wasomaji tutahadhari tusije
tukayachukulia mawazo ya msimulizi kuwa sawa na ya mwandishi kwani wakati
mwingine huwa ni kinyume kabisa.

Tuendelee kuchunguza jinsi Rocha Chimerah alivyoitumia mbinu hii. Katika
riwaya hii, Rocha ameamua kumtumia  mhusika Juma Momanyi kama kinara
anayetuongoza kufuata hadithi yake.  Kwa hivyo, wasomaji twapaswa kuwa
waangalifu tusije tukayachukua maoni, msimamo na imani zote za Juma kuwa
kiwakilishi cha maoni, msimamo na imani za Rocha.

Mbinu hii inapotumika, tunalazimika kufuatilia matukio, kuwafahamu wahusika
wengine na kuielewa hadithi kwa jumla kupitia kwa jicho la huyo mhusika
msimulizi. Msimulizi ndiye anatembea kote na kutufunulia mengi kuhusu
mandhari, wahusika n.k. Kwa mfano, anatufahamisha barabara ilivyo nyumba ya
Omari;

Chumba cha kwanza mkono wa kulia uingiapo ni msala, cha pili ni jiko. Cha
tatu ndicho chumba cha Omari... (uk. 48)
Aidha, ndiye anayetuingiza katika ofisi ya bwana Khalifa na kutufahamisha ilivyo -
mapambo yake na vyote vilivyomo.
Katika uk.1, Juma anatueleza hali ya Omari aliyelala kitandani mgonjwa aso hali
kisha anageukia wengine waliomo mle  chumbani. Katika mbinu hii msimulizi
anafanya jambo moja kwa wakati maalum, kisha akageukia jingine. Tunamtegemea
yeye kuelewa mengi kuihusu hadithi nzima.
Mbinu hii ya usimulizi humbana sana mwandishi. Msimulizi anatueleza na
kutufahamisha yale anayoyashiriki tu (ama kwa kuambiwa, kusikia au kuona). Ni
lazima msimulizi awepo, atueleze. Vinginevyo hatuna namna ya kujua
kinachoendelea pale ambapo msimulizi wetu hajafika. Kwa mfano, kwa vile
hayuko chuoni Gachuka hawezi kutufahamisha yanayoendelea huko. Ndiposa
mwandishi alipohitaji kutufahamisha yanayoendelea huko akalazimika kutumia
barua ya Munga kutujulisha hayo. Pamoja na hayo bado tunamtegemea Juma kwani
hata barua hiyo aliyeandikiwa ni yeye.


54Usimulizi wa Riwaya ya Nyongo Mkalia Ini
Mwandishi anapoeleza jambo fulani mahali maalum, hawezi akaeleza
linaloendelea kwingineko, tofauti na mwakote anayeona na kusikia, pamoja na
kuingia kila mahali. Iwapo mbinu tofauti ingetumika katika riwaya ya Nyongo
Mkalia Ini, mwandishi angeweza kutuhamisha  kutoka Uziwani hadi Gachuka,
akawaacha wa Uziwani kiporo na kutudhihirishia mapambano ya wanafunzi wa
zutafundaki na askari polisi, kisha akaturegesha Uziwani. Angekuwa msimulizi
maizi, yatendekayo sehemu mbalimbali hutufikia kwani msimulizi huyo yu pote
wakati wote.

Matokeo ya matumizi ya usimulizi wa nafsi ya kwanza ni kwamba riwaya hii
imejaa maelezo marefu marefu kuhusu mambo mbalimbali. Yapo maelezo
kuwahusu wahusika kama mama Mumbe, Warega, maumbile yao, sifa, pamoja na
tabia zao mbalimbali. Maelezo kuhusu mandhari ambamo matukio ya hadithi hii
yanatukia, ndoto ndefu ndefu za Juma Momanyi, maelezo kuhusu matukio
mbalimbali ya kihistoria n.k. Tatizo kuu la matumizi ya maelezo marefu sana ni
hatari ya kuwachosha wasomaji wa kazi maalum.

Hata hivyo, mwandishi ameitumia vyema mbinu hii kwa sababu ameichanganya
na ubunifu wake mwenyewe ambao unaipa ubora wa namna yake. Kwanza kabisa,
si Mumanyi tu anayepewa jukumu la kusimulia mambo yote. Kama kawaida ya
kazi mbalimbali za fasihi, kuna mahali kwingi mno ambapo wahusika zaidi ya
wawili wanazungumza kwa kujibizana na hilo si kwa kuendeleza ploti ya riwaya hii
tu bali pia kuwafafanua wahusika wenzao na kadhalika.  Pili, pale ambapo
panahitajika maelezo marefu ya kisimulizi, wapo wahusika wengine ambao pia
wameshirikishwa. Wapo Warega, mama Mumbe, pamoja na Amu Zaid, japo
masimulizi yao ni mafupi kidogo yanapolinganishwa na yale yanayofanywa na
Mumanyi. Kwa mfano maelezo yatolewayo na mama Mumbe na hatimaye mwanae
Warega kuhusu vita vya uhuru na mateso mengi waliyopatishwa wazalendo
yametolewa kwa namna nzuri sana. Maelezo haya yanamteka msomaji na
kumfanya ahisi mpwitompwito mwilini kwa kuwahurumia wale waliojitoa mhanga
kwa ajili ya nchi yao.

Mara kwa mara, katika usimulizi huu wa nafsi ya kwanza, mwandishi ametumia
mbinu ya kuuliza swali au kuulizwa swali; hali nzuri ambayo inatoa fursa kwa wale
wahusika wengine kushiriki kikamilifu hadithini na kukata maelezo ya mfululizo
wa moja kwa moja. Kwa mfano;

Sijaacha kukuuliza. Umesema penye sultani ama mfalme hapana kura...Mbona
huko Ingereza serikali ina vyama viwili vinavyokinzana kila muhula ilhali
twajua Ingereza yatawaliwa na malkia? (uk. 75)
Aidha, matumizi ya barua ya Munga pamoja na ile ya D. Chipuli Dzuya katika
gazeti la 'Baraza' ni namna nzuri sana ya kuchanganya na masimulizi ya moja kwa
moja ili kuendeleza ploti bila kuwakinai wasomaji. Barua hizi vile vile zinatekeleza
jukumu muhimu la kuwaingiza wahusika walio mbali katika hadithi hii.
Swala jingine muhimu linaloibuka katika usimulizi wa Nyongo Mkalia Ini, ni ile
hali ya usimulizi wa kingano ambapo msimulizi ama mtambaji aliwasiliana moja
55Nordic Journal of African Studies

kwa moja na hadhira yake. Katika riwaya hii msimulizi naye, mara kwa mara,
anawasiliana na hadhira yake ya ama wahusika wengine hadithini au wasomaji
wake. Katika uk.16 anawasiliana na wahusika wenzake kwa kusema yafuatayo;
Nyote mwakumbuka vyema siku za mwanzo mama Mumbe alipoingia mjini na
bintiye Warega...

Hili linatukumbusha ule mtindo wa usimulizi wa ngano ambapo msimulizi
alidhihirika wazi wazi mbele ya wasikilizaji wake, akawasiliana nao moja kwa
moja na hata kuwashirikisha katika masimulizi yake ya hadithi. Huu ndio mtindo
ambao wametumia Ama A. Aidoo katika hadithi ya "In the cutting of a Drink"
(1985) pamoja na Ngugi wa Thiong'o katika "A Mercedes Funeral".
Kwingineko riwayani (uk. 47), baada ya kuwasimulia kisa fulani, Mumanyi
anawauliza wahusika wengine waliokuwepo hivi;
Ni nani aliye tayari kukitegua kitendawili hicho?....
Aidha, upo wakati hadithini ambapo mwandishi kupitia kwa msimulizi wake
anajaribu kuwasiliana moja kwa moja na wasomaji wake. Huu hapa mfano wa hali
hiyo;

Tulirudishwa kichekoni. Tulipopoa Warega akachukua uwanja... (uk. 82)
Hapo ni bayana kwamba msimulizi  amejiunga na wahusika wenzake na
kutufahamisha walichokuwa wakikitenda wao kwa pamoja.
Foster (Mlacha 1991) anasema kuwa mwandishi ana uwezo wa kuzungumza
kuhusu wahusika wake au kuzungumza kupitia kwa wahusika wake. Yapo mawazo
mazito, na ya kikauli yanayotolewa  na Rocha kupitia kwa wahusika wake
mbalimbali. Kwa mfano, amemtumia mhusika Munga pamoja na Juma kutoa kauli
madhubuti na za kimsingi sana kuhusiana na imani ya muda mrefu kuhusu watu wa
pwani, ambao yasemekana, ni wavivu. Ukizipitia kauli hizi na zingine kwa makini
hutakosa kung'amua kuwa haya ni mawazo au maoni ya Rocha Chimerah kuhusu
maswala mbalimbali yaihusuyo jamii anayoyamulika katika riwaya yake.
Dosari moja kuu ninayoiona kuhusiana na usimulizi wa nafsi ya kwanza ni
kwamba mbinu hii yaweza kukinai na kuchosha, tofauti na nyingine ambazo
zinatoa nafasi kubwa kwa watu wengi  kushiriki kuiendeleza hadithi. Hili
linajitokeza katika Nyongo Mkalia Ini, hasa pale ambapo mwandishi anatumia
msimulizi wake kutuelekeza kutizama mambo anavyotaka yeye. Kwa mfano;
Sasa hebu niifungue nione ananieleza kisa gani... (uk. 15)

Hapa, msimulizi anatuelekeza na kutuongoza, hali ambayo inaikatisha furaha yetu
kama wasomaji ambayo tungeipata iwapo angeendelea na masimulizi kisha sisi
wenyewe tuunge vijisehemu vijitokezavyo na hivyo kujigundulia mshikamano wa
kadhia yake.

Katika uk. 45, msimulizi wa Nyongo Mkali Ini anatoa maelezo kuhusu swala la
nyuki walao asali, pamoja na ile ndoto yake. Juma anayahitimisha maelezo hayo
hivi:
56Usimulizi wa Riwaya ya Nyongo Mkalia Ini
Mja...nyuki...Samahani ndugu; huo ndio utakao kuwa mwisho wa maelezo
yangu juu ya nyuki...

Ufafanuzi huo haukuwakolea wasikilizaji wake; nao wakataka maelezo zaidi. Bila
kusita akajibu;

Haya basi nitajaribu kufafanua zaidi...Sisi sote ni nyuki. Kama nyuki
tumegawanyika matabaka matabaka. Kama nyuki, wapo wanaochuma asali na
wanaokula asali. Ni wajibu wa kila... afadhali tutie kikomo hapo. (uk. 46)
Ukweli ni kwamba hii kauli yake inadhihirisha vizuri sana namna ambavyo jamii
yetu imegawanywa katika matabaka huku wachache wanafurahia jasho la wengi.
Kwa hilo, sawa kabisa, lakini ingekuwa bora kama angetufumbia na kutuacha
wenyewe kujijazia. Unapofumba na kisha ukataka kutanzua au kulifumbua fumbo,
ile raha ya fasihi inakuwa haipo tena. Ingawa anaghairi kuendelea kulifafanua
fumbo lake; hivyo kutuachia jukumu letu kama wasomaji, hafanyi hivyo kwa
sababu anaamini si vizuri, bali kwa sababu, kama asemavyo mwenyewe; "hata
nyasi zina masikio". Ni maswala nyeti ambayo hayapaswi kuelezwa wazi wazi.
Tatizo jingine ni lile la msimulizi  kutoa maelezo mengi kujihusu. Katika
kuwafafanua wahusika, mbinu ya mhusika kujieleza mwenyewe si nzuri sana kwa
sababu huenda akatuficha mengi ambayo hataki tuyajue kama ilivyo kawaida ya
mwanadamu. Hii hapa mifano miwili ya jinsi msimulizi anavyojitathmini:
Kwa kawaida huwa sipendi kuingiaingia mabaani...na mimi sipendezwi na baa
yoyote hata kama ina sifa za uzuri wa peponi. (uk. 8)

... sijisifu, lakini kwa kuwa ni mwenye kupenda ukweli, nasema kweli... (uk. 1)
Utaona kuwa msimulizi anatueleza yale  atakayo yeye, sisi tuyajue na kuacha
asiyoyataka. Kwa kufanya hivyo, anatuelekeza katika mkondo maalum wa mawazo
anaoupendelea yeye. Japo anaonya kwamba hajisifu; ukweli ni kwamba ndivyo
anavyofanya. Ingekuwa bora kama tungepata kukaulisha kuhusu hulka yake na sifa
zake mbalimbali kutokana na maingiliano yake na wahusika wengine hadithini,
matendo yake, pamoja na wanayoyasema wahusika wengine badala ya kuambiwa
naye. 57Nordic Journal of African Studies

4. HITIMISHO
Kwa jumla, pamoja na matatizo mbalimbali yanayoambatanishwa na mbinu hii ya
usimulizi, mwandishi wa riwaya hii ameitumia vizuri. Ameweza kutumia ubunilizi
wake mwenyewe kuepuka ukinai wa usimulizi wa nafsi ya kwanza. Amefanya la
busara pia kuwapa wahusika wengine kando na Juma (msimulizi mkuu), nafasi ya
kusukuma mbele hadithi yake. Hali hii tunaishuhudia zaidi wakati wa majadiliano
marefu yanayowakutanisha Munga, Obote, Omari, Warega, pamoja na Mumanyi
mwenyewe.

Hilo pamoja na matumizi mazuri ya hadithi za mama Mumbe, maelezo ya
Warega pamwe na zile barua zipatikanazo katika riwaya hii linaipa kazi hii upekee
katika matumizi ya usimulizi wa nafsi ya kwanza. Aidha, hayo yamemsaidia
mwandishi kuepuka tata mbalimbali na ukinai wa usimulizi wa nafsi ya kwanza,
hasa itokeapo kwamba usimulizi huo haujachanganywa na mbinu nyingine zozote
wala kuambatanishwa na ubunifu wa mwandishi husika.

0 comments:

Post a Comment