Menyu

Swahili Hub

Ati, binadamu amegeuka na kuwa nguruwe?



wakati mwengine binadamu – yule kiumbe mwenye akili sana mpaka akajipachika cheo cha “U-Homo Sapiens” – anaweza kukushangaza na kukufanya uusaili ubinadamu wake. Na hapa sizungumzii vita au matatizo yake mengine anayojisababishia. Hebu soma kisa hiki kifupi.


Kama ilivyo kawaida yangu, jana asubuhi ilikuwa siku yangu ya kwenda kujitolea kufundisha sayansi kwa wanafunzi wa darasa la tatu katika shule mojawapo ya msingi hapa ninapoishi. Darasa langu lilikuwa la masaa matatu (2:30 – 5:30 asubuhi). Ili kukwepa msongamano wa magari, nilijidamka mapema na kwenda kusubirisha darasa langu katika MacDonald’s mojawapo iliyo karibu na shule. Hapo nilinunua kahawa na kuanza kufanya kazi katika kompyuta yangu.







Baada ya muda alifika mzee mmoja mtanashati ambaye ilikuwa dhahiri kwamba alikuwa mgonjwa. Mbali na mikono yake kutetemekatetemeka, miguu yake ilikuwa imevimba na alikuwa anatembea kwa shida kidogo. Mzee yule alikuja na kukaa mbali kidogo nami. Nilimsikia akijaribu kuwaomba watu waliokuwa karibu naye wamsaidie angalau dola mbili hivi  ili akanunue maji ya machungwa. Watu wote waliokuwa karibu naye walisema kwamba hawakuwa na kitu na wengine walikaa kimya tu bila kumjibu. Basi mzee yule alibakia tu amekaa pale huku watu wote waliomzunguka walikuwa wamekazana kutafuna kifungua kinywa chao bila wasiwasi.

Mandhari yale yalinishangaza sana. Inakuwaje binadamu mwenye ubinadamu wake akae pale na kujaza tumbo lake wakati binadamu mwenzake tena mgonjwa anayehitaji glasi moja tu ya maji ya machungwa akiwa hana kitu? Ubinadamu wa binadamu uko wapi?

Sipendi kusema nilichokifanya lakini kisa hiki kilinifanya niufikirie upya mustakabali wa binadamu na migongano yake ya kitabaka na kiamali. Ni nini kinachomfanya aliyenacho ashindwe kutambua shida za asiye na cho chote – hata kama huyu asiye nacho yupo katika mateso na hali ngumu kama ya huyu mzee, hali inayotosha kuchochea moto wa ubinadamu katika moyo wa aliyenacho? Ati, ni nini kinachomfanya fisadi asijisikie vibaya anapoiba mali za wanyonge wasiona na cho chote na kuendeelea kujitajirisha yeye na familia yake wakati binadamu wenzake wakiendelea kusikinika? Ubinadamu wa binadamu uko wapi? Au pengine ule msemo wa Kiingereza kwamba “Human beings are overrated” ni wa kweli?

Hebu basi na tukajaribu kuuruhusu ubinadamu wetu ukachomoze – hata kwa mambo madogomadogo kama haya ya kumsaidia mzee mgonjwa anayehitaji glasi moja tu ya machungwa katika asubuhi nzuri kama ya jana. Wikiendi njema !!!


1 comments:

  1. Kisa na visa vyako huwa ni vya kusisimua sana. Jinsi unaitumia lugha maridhawa na mufti, hunitia ilihamu pia. Nashukuru sana kaka kwa kutujuza mengi

    ReplyDelete