Kipindi cha miaka mitatu ni kifupi, lakini hifadhi hii imeweza kuleta sifa kubwa kwa nchi hii, kutokana na kuweza kuvutia wageni wengi wa ndani na nje ya nchi.
Tangu ibadilishwe na kuingizwa chini ya hifadhi za taifa, mbuga hii ya wanyama ya Mkomazi imeweza kutembelewa na wageni zaidi ya 1,100 ambao kwa nyakati tofauti wameweza kufika katika hifadhi hiyo kujionea vivutio mbalimbali.
Meneja uhusiano wa Hifadhi za Taifa (Tanapa), Pascal Shelutete anasema, katika kipindi cha miaka mitatu tangu waanze kuisimamia hifadhi hiyo wamekuwa wakiwekeza nguvu nyingi katika kuboresha miundombinu ya ndani ya hifadhi ili maeneo ya ndani ya hifadhi yaweze kufikika kwa urahisi.
Shelutete anasema wakati wanakabidhiwa hifadhi hiyo wakati huo ikiwa chini ya pori la akiba, ilikuwa ikikabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na ukosefu wa miundombinu thabiti ya kuwezesha eneo la hifadhi kufikika kiurahisi.
Mbali na tatizo la miundombinu anasema, kulikuwa na tatizo na malisho ya wanyama hasa upatikanaji wa maji kwa ajili ya wanyama waliopo eneo la hifadhi ambayo tanapa imeanza kuyaondoa.
“Tanapa tupokabidhiwa hifadhi hii tulikuta tatizo moja kubwa la wanyama kukimbia hifadhi za nchi jirani ya Kenya kutokana na ukame…tatizo la maji ya kunywa kwa wanyama lilikuwa kubwa na lilisababisha wanyama wengi kukimbilia nchi hiyo jirani…lakini tangu tumeanza kuisimamia hii hifadhi tulianza kutatua tatizo hili, na sasa hali ni nzuri na maeneo mengi katika hifadhi maji yanapatikana” anasema Shelutete
Je, ni jitihada gani zilizofanywa na Tanapa kufanikisha upatikanaji wa maji katika hifadhi hiyo?
Mhifadhi Utalii wa hifadhi hiyo, Beatrice Ntambi anajibu kwamba katika kukabiliana na tatizo hilo la wanyama kuikimbia hifadhi hiyo, Tanapa, imefanikiwa kujenga mabwawa kwa ajili ya kuhifadhi maji ya kunywa yatakayotumiwa na wanyama.
“Tumejenga mabwawa matano sehemu mbalimbali katika hifadhi, haya yamesaidia kurejesha wanyama waliokuwa wakikimbilia Kenya kufuata maji kutokana na ukame uliokuwepo hifadhini miaka ya nyuma” Anasema.
Anasema mabwawa hayo yanajazwa maji kwa kutegemea mvua na kwamba pango wa mamlaka hiyo ni kujenga mabwawa mengi zaidi yatakayoiwezesha hifadhi hiyo kuwa na uwezo wa kuwanywesha wanyama pori kwa kadri ya mahitaji halisi.
Mkomazi ipo wapi?
Hifadhi ya Mkomazi ipo katika mikoa miwili ambayo ni Kilimanjaro na Tanga, ndani ya Wilaya za Same na Lushoto.
Sifa ya pekee ya Mkomazi, pengine kuliko hifadhi nyingi za taifa za nchini, ni kufikika kwa urahisi. Hifadhi hii ipo kilometa mbili kutoka barabara kuu ya Moshi-Arusha.
Mhifadhi Mkuu wa hifadhi hiyo, Donat Mnyagatwa anasema, Mkomazi inayo sifa ya ziada ambayo ni kufikika kwa urahisi kutokana na kuwa jirani na barabara kuu.
Anasema sifa nyingine kubwa ambayo pengine ndio kivutio cha pekee cha hifadhi hiyo ya taifa ni kuwa na wanyama wasiopatikana kwa wingi katika maeneo mengi ya hifadhi.
“Mkomazi wapo wanyama wa pekee kama Swala twiga na cholowa, hawa ni vivutio ambavyo wageni wengi wakija hufurahia kuviona..pia tunao simba, twiga, tembo, pundamilia na mbwa mwitu ambao nao ni kivutio kikubwa kutokana na kuwa wengi kwa makundi.” Anasema
Mnyagatwa anasema hifadhi ya hii ilianzishwa mwaka 1951 kama pori la akiba likiwa limetengwa kutoka katika pori kubwa la akiba la Ruvu.
Hifadhi hii ina ukubwa wa kilometa za mraba 3,245 na kwamba pori hilo lilipendekezwa kuwa hifadhi ya taifa kwa misingi ya kunusuru maeneo na rasilimali zilizomo kutokana na matumizi yasiyoendana na uhifadhi kwa ajili ya kizazi kijacho.
Anasema mbali na wanyama, zipo takribani aina 450 za ndege wa aina mbalimbali ikiwa ni pamoja vifaru weusi walioingizwa kutoka kutoka nchi za Afrika kusini na Uingereza.
Mnyagatwa anaongeza kuwa faru waliopo sasa wanahifadhiwa kwa uangalizi na ulinzi mkubwa, wakipewa nafasi ili waongezeke idadi yao kufikia inayoruhusiwa kwa shughuli za utalii.
Anasema serikali inatumia mbinu tofauti kuhakikisha faru hao ambao ni miongoni mwa wanyama wanaowindwa na majangili duniani kote, wanapata ulinzi madhubuti.
Anasema ulinzi dhidi ya faru hao unafanyika, kwa kutegemea wadau mbalimbali, lakini zaidi ni Watanzania wanaoguswa na rasilimali hiyo yenye maslahi kwa umma.
“Tunao vifaru ambao nao wanaongeza kuifanya mbuga yetu iwe kivutio zaidi…faru hawa ni mchanganyiko na wale walioletwa kutoka nchini Uingereza ambao tunajitahidi kuwatunza na kuwalinda ili idadi yao iongezeke” anasema Mnyagatwa.
Mkakati wa kuongeza watalii
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Allan Kijazi, anasema licha ya bahati kubwa iliyopo kwa Tanzania kuwa na vivutio vingi vya utalii katika dunia, ni bahati mbaya sana kuwa baadhi ya wananchi bado hawajapata elimu ya umuhimu wa kutembelea vivutio hivyo.
Anaongeza kuwa watanzania walio wengi hawana utamaduni wa kutembelea maliasili zao na akasema tanapa imekuwa na mikakati ya mara kwa mara ya kuwawezesha wananchi kutembelea hifadhi zake kwa urahisi na kwa bei nafuu.
“Kiingilio cha kuingia katika hifadhi ni shilingi 2000 kwa mtanzania na 500 kwa mtoto, pia tumekuwa utaratibu wa kuandaa usafiri nyakati za sikukuu na hata wakati wa maonyesho ya sabasaba ambapo wananchi wengi huhamasika kutembelea hifadhi hizo kutokana na gharama nafuu” anasema Kijazi.
Anasema moja ya changamoto wanayokabiliana Tanapa katika hifadhi zake ni gharama kubwa katika malazi ambapo anasema ili kukabiliana na changamoto hiyo, wamekuwa na mpango wa kuweka malazi ya bei nafuu ndani ya hifadhi.
Kuhusu kuongeza watalii wa nje, Kijazi anasema Tanapa imekuwa ikijitahi kutangaza vivutio vilivyopo ndani ya hifadhi zake ndani na nje ya nchi, ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu na malazi katika maeneo ya hifadhi ambayo kwa kiasi kikubwa yamechangia kuongeza idadi ya watalii wa nje.
<<<<
0 comments:
Post a Comment