Menyu

Swahili Hub

Uingereza, New Zealand kufungua Olimpiki


TIMU ya taifa ya wanawake ya soka ya Uingereza inatarajiwa kupata ushindi mkubwa katika mechi ya leo ya ufunguzi wa michezo ya Olimpiki dhidi ya New Zealand. Mechi hiyo inachezwa leo ikiwa ni siku mbili kabla ya ufunguzi rasmi wa michezo ya Olimpiki ambayo ni michezo mikongwe duniani.


"Timu yetu inatarajiwa kuliweka soka letu la wanawake juu, inatarajiwa kuliweka soka letu katika ramani ya soka duniani na tuna imani tutapata ushindi mkubwa katika mechi yetu hii,"alisema kocha wa timu ya wanawake ya Uingereza, Hope Powell.

Alisema,"hii ni mara ya kwanza kwa timu yetu ya wanawake kushiriki michezo ya Olimpiki, najua Waingereza wana wasiwasi na timu yetu, lakini naamini tutafanya vizuri."

Kocha Powell alisema,"mechi hii ni muhimu kwetu na ninatarajia itakuwa mechi nzuri na tutapata matokeo mazuri pia."

"Kutakuwa hakuna michezo mingine itakayofanyika kesho (leo) hivyo natarajia vyombo vya habari vitakuwa vinaifuatilia mechi hii,"alisema kocha Powell.

Mshambuliaji wa timu ya Birmingham City anayeichezea timu ya wanawake ya Uingereza, Eniola Aluko ambaye alikuwapo katika mechi ya kirafiki dhidi ya Sweden Ijumaa iliyopita alisema anaamini timu yao itatoa nafasi katika kuwavutia wasichana wengi wa Uingereza kushiriki katika mchezo wa soka.

"Ni heshima kubwa kwetu kuiwakilisha timu ya Uingereza, siyo kitu cha mchezo kuchaguliwa kuunda kikosi cha watu 18 cha timu ya wanawake ya Uingereza hivyo watu wengi wanatarajia tutacheza kwa ushindani na kuvutia wasichana wengi kushiriki katika mchezo wa soka, hii ni heshima kubwa kwetu,"alisema Aluko.

Timu ya Uingereza 


Timu ya Uingereza inayonolewa na Powell ipo kundi E pamoja na timu kali ya Brazil, Cameroon na timu ya New Zealand.

Timu mbili katika kila kundi zitakazoshika nafasi za juu zitafuzu kuingia hatua ya robo fainali, pia timu mbili zitakazoshika nafasi ya tatu zitaingia katika hatua hiyo ya robo fainali.

Katika mechi za wanawake za soka katika michezo ya Olimpiki hakuna suala la kuangalia umri kama lilivyo kwa upande wa soka kwa wanaume katikia michezo ya Olimpiki.

Timu ya Uingereza ya wanawake itacheza mechi ya pili katika michezo huyo dhidi ya Cameroon siku ya Jumamosi huko Cardiff na itamalizia mechi za hatua ya makundi kwa kucheza dhidi ya Brazil kwenye Uwanja wa Wembley.

<<<<Swahili Hub

0 comments:

Post a Comment